Mwigulu aruhusiwa kutoka hospitalini

Muktasari:

Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa amelazwa Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma ameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya afya yake kuimarika.


Dodoma. Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa amelazwa katika hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kupata ajali ameruhusiwa kutoka hospitalini hapo.

Dk Mwiguli alipata ajali Februari 13, 2019 katika eneo la Migori mkoani Iringa akitokea mkoani humo kwenda mkoani Singida baada ya gari lake kugonga punda waliokuwa wanakatisha barabara.

Katika ajali hiyo Dk Mwigulu, aliumia maeneo ya kifua, nyonga na kwenye mguu lakini dereva wake ambaye ni mtu pekee aliyekuwa naye kwenye gari hilo hakuumia mahali popote.

Leo Februari 15, 2019 mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Alphonce Chandika amesema waziri huyo wa zamani wa mambo ya ndani ameruhusiwa hospitalini hapo baada ya afya yake kuimarika.

“Mheshimiwa Mwigulu anaendelea vizuri na sasa tumemruhusu kurejea nyumbani baada ya afya yake kuimarika,” amesema Dk Chandika.