Mwili wa Godzilla kuagwa sehemu tatu tofauti

Thursday February 14 2019

 

By Rhobi Chacha, Mwananchi

Dar es Salaam. Mwili wa msanii maarufu wa muziki wa Hip Hop, Godzilla huenda akaagwa katika maeneo matatu tofauti Jumamosi Februari 16.

Staa huyo wa muziki wa rap nchini, alifariki dunia jana baada ya kuugua kwa siku tatu mfululizo.

Akizungumza na MCL Digital ,baba mlezi wa Godzilla, Antony Kato amesema hapo awali walipanga bajeti ya mazishi Sh6 milioni lakini sasa imeongezeka kufikia Sh8 milioni baada ya wasanii kuomba aagwe katika viwanja vya Leaders, jijini Dar es Salaam.

Kato amesema familia ilipanga Godzilla aagiwe nyumbani kwao Salasala na baadaye kanisani, lakini limejitokeza suala la wasanii wenzake kuomba aagiwe Leders.

Hata hivyo, Kato amesema leo jioni watakaa kikao na  kuamua kama itawezekana Godzilla mwili wake ukaagwa sehemu tatu ambazo ni nyumbani, kanisani na Leaders sababu watu wote wana umuhimu kwake.

“Tunataka kila mtu ashiriki katika karamu ya mwisho ya kijana wetu, tunafikiria namna ya kuhakikisha watu wake wa karibu wanapata nafasi ya kumuaga kama walivyoomba, mipango ikikaa vizuri ataagwa sehemu zote tatu,” amesema Kato.

Godzilla amefariki dunia usiku wa kuamkia Jumatano Februari 13, 2019 majira ya saa 10 alfajiri nyumbani kwao Salasala jijini Dar Es Salaam, baada ya kusumbuliwa na malaria, sukari na shinikizo la damu.


Advertisement