Mwili wa mfanyabiashara maarufu, Askofu Mollel kuwasili Arusha Jumapili.

Muktasari:

Mfanyabiashara madini Askofu Mollel aliyefariki dunia akiwa mkoani Dodoma, utazikwa Jumatatu huku wachimbaji wakimlilia.

Arusha. Mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite nchini, Thomas Mollel maarufu kama ‘Askofu’ aliyefariki ghafla jijini Dodoma,  anatarajiwa kuzikwa Jumatatu katika Kijiji cha Mbuguni Wilaya ya Arumeru.

Mollel ambaye alikuwa Dodoma kumsindikiza kuapishwa mbunge wa Jimbo la Arumeru Mashariki, John Pallagyo anatarajiwa kusafirishwa  Jumapili kutoka Dodoma.

Katibu Mwenezi wa CCM Wilayani Meru, Joshua Hungura amesema mwili wa mfanyabiashara huyo utasafirishwa kwa ndege hadi uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Jumapili ya Mei 26,2019.

Amesema kikao kilichofanyika kati ya  familia ya Mollel na viongozi wa CCM,  wamekubaliana azikwe Jumatatu, Mei 27, 2019.

Hungura amesema Mollel ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM wilaya ya Meru na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ataagwa nyumbani kwake Mbuguni.

Katika uhai wake, Mollel alikuwa mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite na aliwahi kumiliki timu ya mpira iliyowahi kushiriki Ligi kuu ya Pallson aliwahi kuwa diwani wa CCM Kata ya Mbuguni.

Sadiki Mnenei ambaye alikuwa mwenyekiti wa chama cha wachimbaji wa madini Mkoa wa Manyara, amesema kifo cha Mollel ni pengo kwa wachimbaji.

“Alikuwa mchimbaji wa siku nyingi na amesaidia sana sekta ya madini, ameacha pengo,” amesema Mnenei.