Mwili wa mke wa Askofu wa kwanza KKKT waagwa Azania Front

Muktasari:

Mwili wa mke wa mkuu wa kwanza wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Stephano Moshi, umeagwa leo mchana Machi 24 katika Kanisa Kuu la Azania Front misa iliyohudhuriwa na washarika wengi wa kanisa hilo

Dar es Salaam. Mwili wa mke wa Askofu wa kwanza wa Kanisa la KKKT, Ndeambiliasia Moshi umeagwa leo katika Kanisa Kuu la Azania Front katika misa maalum iliyohudhuriwa na waumini wengi wa dhehebu hilo.

Mwili huo unatarajiwa kusafirishwa leo, Machi 24 kuelekea nyumbani kwake Marangu, Mamba Kotela, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Akitoa mahubiri wakati wa ibada hiyo, Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa ametaka wafiwa kusherehekea maisha ya Ndeambiliasia badala ya kuomboleza.

“Ninamfahamu huyu bibi kwa kuwa ni mtu ambaye alikuwa ana upendo mkubwa sana na furaha wakati wote, ukifika kwake hutaondoka mikono mitupu, hivyo leo ni siku ya furaha hatutaki kuhuzunika kwa kuwa angeendelea kuishi mpaka lini?

“Kumbukeni miezi mitatu iliyopita na mfurahie siku mlipotoa sadaka ya pekee wakati mpendwa wenu alipotimiza umri wa miaka 100, shukuruni kwani hatujui nani atafuata baada ya mpendwa wetu, sote ni wa kwake na kwake tutarejea,” amesema Askofu.

Akitoa salamu za rambirambi, kiongozi wa wake za wachungaji alisema, “Mama alipenda sana kuwashauri wake za wachungaji na alipenda kuwaunganisha.”

Akisoma wasifu mtoto mkubwa wa marehemu, Zebedayo Moshi amesema marehemu Ndesambiliasia Moshi alifariki Machi 20 jijini Dar es Salaam na anatarajiwa kuzikwa Machi 25 nyumbani kwake Marangu Moshi.

Alisema marehemu alizaliwa Desemba 15 mwaka 1918 na kufariki akiwa na umri wa miaka 100 na miezi mitatu.

Mama Askofu Moshi amefariki dunia ikiwa ni zaidi ya miaka 40 tangu mumewe Dk Stephano Moshi aliyefariki mwaka 1976 akiwa bado ni mkuu wa KKKT.

Bibi Ndesambiliasia ni mke wa pili wa Askofu Dk Moshi baada ya kufariki kwa mkewe wa kwanza. Akiwa katika ndoa hiyo, walijaaliwa kupata watoto watatu ambao ni Maria, Dora na Zebadia.

Mbali na watoto hao, kwa miaka yote ya uhai wake pia amekuwa na jukumu la kuwalea watoto wengine watano wa mtangulizi wake katika ndoa hiyo ambao ni John, Hosea, Joshua, Iriaeli na Aimtonga.

Ameacha watoto sita, wajukuu 39, vitukuu 79 na vilembwe 27 na kwa mujibu wa wanafamilia bibi huyo alifikisha uzao wa watu 150 katika familia yake.