Mwili wa mwanafunzi wakutwa karibu na shule

Saturday March 16 2019

By Rehema Matowo, Mwananchi [email protected]

yang’wale. Mabaki ya mwili wa mwananfunzi wa kidato cha kwanza katika Sekondari Nyungwa wilayani hapa, Alex Pastory (16), aliyetoweka siku nane zilizopita yamekutwa mita 500 kutoka shuleni hapo.

Alex aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha, mabaki ya mwili wake yamepatikana baada ya mwanamke aliyekuwa akilima shambani kukuta fuvu la kichwa, sare za shule na soksi vilivyotambuliwa kuwa ni mavazi ya mwanafunzi huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema jana kuwa wanaendelea na uchunguzi kujua chanzo cha kifo chake.

Kwa mujibu wa kamanda huyo, Alex aliyekuwa anaishi mwenyewe kwenye chumba cha kupanga alikuwa mgonjwa na Januari 28 aliomba ruhusa shuleni ya kwenda kwao na kurudi Februari 28, ambapo Machi Mosi alihudhuria vipindi darasani hadi wakati wa mapumziko, lakini hakuonekana tena.

“Walimu walitoa taarifa na kuwasiliana na familia lakini hakupatikana, ambapo wazazi walifika Machi 3 na kujumuika na wanafunzi wengine kumtafuta bila mafanikio hadi mama mmoja alipokutana na fuvu la kichwa wakati akilima shambani,” alisema.

Alisema baada ya kukutwa kwa fuvu hilo wananchi walianza kutafuta mabaki ya mwili na kukuta sare za shule ambazo zilifanya watambue kuwa ndiye mwanafunzi wa shule hiyo aliyetoweka.

Mwabulambo alisema kwa sasa wanafanya uchunguzi kwa wanafunzi wenzake, marafiki na mwalimu wa darasa ili kujua kama alisema jambo lolote baada ya kurejea kutoka nyumbani kwao. Mabaki ya mwili wa mwanafunzi huyo yamechukuliwa na wazazi wake wanaoishi Ukerewe mkoani Mwanza kwa ajili ya maziko

Advertisement