Mwimbaji asimulia siku 227 za mjukuu wake wodini

Muktasari:

  • Mwimbaji wa taarabu aliyewahi kutamba na wimbo ‘Njiwa Peleka Salamu’ Patricia Hillary amesimulia namna alivyomuuguza mjukuu wake Hillary Plasdius (8) siku 227 katika Hospitali ya Muhimbili – Mloganzila aliyepata ugonjwa nadra kupatikana kwa binadamu na kuwekwa chumba cha uangalizi maalum (ICU) miezi minne akitumia mashine ya kumsaidia kupumua.

Dar es Salaam. “Nilifika hapa Hillary alikuwa na hali mbaya, nilikuwa nimechanganyikiwa na kukata tamaa, kila mmoja aliwaza na kuuliza kutakucha… hakuna aliyejua mwisho utakuwaje,” anaanza kusimulia Patricia Hillary.

Oktoba 29 mwaka 2018, Hillary ambaye mwaka 2019 alitakiwa kuanza darasa la kwanza aliugua ghafla na kupooza mwili mzima, kufuatia seli za mwili wake kupambana zenyewe ugonjwa ambao ni nadra kuwapa watu wazima na watoto.

Akizungumza jana Jumatano Juni 12, 2019 baada ya mjukuu wake, Hillary Plasdius (8) kuruhusiwa kurudi nyumbani, Patricia amesema japokuwa ugonjwa huo hawakuufahamu ilikuwa ni vigumu kuuguza kwani ilifikia hatua walikata tamaa.

“Namshukuru Mungu aliyeweka mkono wake kwa mjukuu wangu, wapo waliozungumza kuwa hakuna mtu tena kutokana na hali aliyofikia, nilisema nina imani madaktari na Mungu tunayemuamini Hillry atainuka pale alipo na kutembea hawakuamini baadhi yao wamekuja kumuona hivi alivyo sasa wananikumbatia na kulia.”

“Nawashukuru madaktari, viongozi, wafanyakazi wote tulionyeshwa upendo mkubwa, wametoa dawa zimemsaidia huyu mtoto nasikia faraja sana leo. ICU nimekaa nao muda mrefu wananipa faraja kubwa sana, wametoa dawa mpaka leo Hillary tupo naye,” amesema Patricia.

Mkuu wa Kitengo cha watoto na Daktari Bingwa wa Watoto Mloganzila, Mwanaidi Amiri amesema Hillary alipata maambukizi ya kifua, kwenye mfumo wa hewa au mfumo wa chakula yaliyosababishwa na bakteria na kusababisha mwili kushambulia mishipa ya fahamu na kusababisha misuli kukosa nguvu kwani ilianzia miguuni na kupanda mpaka shingoni na akapooza.