Mzalishaji mvinyo wa Tanzania apata soko Afrika kusini, Zimbabwe

Thursday August 8 2019

 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam.  Yusuph Lukiko, mmiliki wa kampuni ya kuzalisha kilevi kisichokuwa na kemikali amepata soko la kuuza bidhaa zake Afrika Kusini na Zimbabwe kupitia maonyesho ya bidhaa za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika( SADC).

Lukiko(34) ambaye kiwanda chake kilichopo nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam,  huzalisha lita 600 za bia kwa mwezi.

Aliacha kazi mwaka 2016 baada ya kupata mafunzo ya uchachuaji wa pombe zisizokuwa na kemikali. Anatumia tanki nane za kusindika kwa siku saba. 

Anachachua aina nane za bia kwa kiwango cha nyuzi joto chini ya 23 ambacho kinasaidia uhai wa kilevi hicho kwa muda wa zaidi ya miezi sita bila kuharibika. Bia zake zina kiwango cha asilimia 4.4 ya kilevi.

Akizungumza na Mwananchi i katika maonyesho ya bidhaa ya SADC yanayoendelea kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere,  Lukiko amesema mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya Bisto ya Afrika Kusini ilimtembelea jana kwa ajili ya mazungumzo yaliyoonyesha matunda.

“Wamekuja na tumezungumza, kikubwa wamechukua sampuli na wamedhamiria kuunganisha ubia wa kampuni zetu ili kuwekeza katika soko la Afrika Kusini, wamevutiwa na ladha ya bia zangu na wamesema zitakuwa na soko kubwa nchini kwao, “amesema Lukiko.

Advertisement

Lukiko amesema kampuni nyingine ambayo hakutaka kuitaja jina ni ya  Zimbabwe iliyopo katika maonyesho hayo.

“Hawa Wazimbabwe wamesema kwanza wanahitaji nikafundishe namna ya kuzalisha bia hii lakini pia watakuwa soko langu nchini Zimbabwe. Siyo muda sahihi wa kueleza haya masuala kwa kina katika media,” amesema.

Mwaka 2018 Lukiko alishinda tuzo ya kuwa mzalishaji bora wa bia nchini Afrika Kusini, ambayo mwaka huu imechukuliwa na Kampuni ya bia ya TBL ya Tanzania.

Lukiko alianza kujihusisha na utundu wa kujifunza zaidi kuhusu uzalishaji wa bidhaa hiyo baada ya kuanza kazi katika kampuni ya SBL, akiwa na elimu ya cheti mwaka 2009 lakini aliamua kujiunga Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) akichukua shahada ya uchakataji wa matunda(food processing).

“Nilimaliza mwaka 2012 na kuendelea na kazi SBL, lakini mwaka 2015 nilikwenda Afrika kusini kwenye mafunzo ndiko nikaanza kufikiria kuacha kazi ili nianze kuzalisha mwenyewe. Nikafuatilia mbinu za kuzalisha zaidi kwa rafiki yangu mmoja Kenya aliyenitumia flash ya materials, nikaanza kujisomea Youtube hadi nikamaliza na kuanzisha rasmi kiwanda ndani ya chumba ninapoishi,” amesema.

Hata hivyo, amesema kabla ya kuanza rasmi kufanya biashara alitumia muda wa mwaka mmoja kupata vibali na nyaraka za kufanya biashara hiyo kutoka mamlaka husika za Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na TFDA ambayo sasa inaitwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).

Advertisement