Mzazi wa aliyeozwa udogoni matatani

Friday January 10 2014

By Ahmed Makongo, Mwananchi

Bunda. Mzazi anayedaiwa kumuoza mtoto wake kwa mwanamume mwenye umri wa miaka 54, amekamatwa na polisi na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Bunda.

Mzazi huyo amefunguliwa kesi ya kula njama kwa nia ya kutenda kosa la kuozesha mtoto mdogo isivyo halali.

Aliyefikishwa katika mahakama hiyo iliyoketi chini ya hakimu Ahmed Kasonso, ametajwa kuwa ni Kakwaya Monge (53) mkazi wa Kijiji cha Nyaburundu wilayani humu.

Jana ilielezwa mahakamani kwamba mtoto ambaye awali alidaiwa kuwa na umri wa miaka minane, umri wake halisi ni miaka 12.

Maelezo hayo yalikuja baada ya mzee aliyemuoa, Changwe Changigi (54) naye kufikishwa katika mahakama hiyo na kushtakiwa kwa makosa yote matatu, likiwemo la kubaka.

Mwendesha Mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Masoud Mohamed, alidai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya kula njama kwa nia ya kutenda kosa.

Advertisement

Mohamed alisema mzee anayetuhumiwa kuoa mtoto huyo, anashtakiwa kwa makosa ya kubaka na kuoa mtoto mdogo kinyume cha sheria.

Alisema washtakiwa walitenda kosa hilo Januari mosi mwaka huu katika Kijiji cha Nyaburundu.

Juzi katika mahojiano na Dawati la Jinsia katika Kituo cha Polisi cha Bunda, mzazi huyo, alisema aliamua kumuoza kwa sababu alikuwa anaumwa moyo.

Alisema Sh55,000 alizopewa kama kishika uchumba, zilimsaidia kununua dawa za ugonjwa huo.

Advertisement