Mzee Yusuf kuwasomea dua waliomvamia ili wateseke

Muktasari:

  • Siku chache baada ya kuvamiliwa na watu wasiojulikana  nyumbani kwake Chanika  jijini Dar es Salaam, mwalimu wa dini aliyewahi kuwa mwimbaji wa muziki wa taarabu, Mzee Yusuf amesema anasoma dua ya saa tatu kwa ajili ya wavamizi hao

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kuvamiliwa na watu wasiojulikana  nyumbani kwake Chanika  jijini Dar es Salaam, mwalimu wa dini aliyewahi kuwa mwimbaji wa muziki wa taarabu, Mzee Yusuf amesema anasoma dua ya saa tatu kwa ajili ya wavamizi hao.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Januari 11, 2019 Mzee Yusuf amesema hatawaacha waliomvamia, atasoma dua itakayowahukumu kwa kitendo hicho. 

Amesema dua si albadiri, kwamba ni ya kawaida ambayo itawatesa waliompa mateso yeye na familia yake.

"Msema kweli mpenzi wa Mungu, siwezi kuwaacha wanipe hasara, wamjeruhi mke wangu na mwanangu halafu wadundike mitaani Nasema wazi nitakaa chini kwa saa tatu kusoma dua kwa ajili yao, lazima wapate mateso kama tuliyoyapata sisi,” amesema Mzee Yusuf.

Yusuf alivamiwa Januari 7, 2019 nyumbani kwake Chanika Buyuni Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam,  wavamizi hao walimjeruhi  mkewe Leyla Rashid sehemu mbalimbali mwilini na kuiba saa, pete moja, viatu, simu  na pesa.

Leyla alilazwa hospitali baada ya kupata majeraha ila kwa sasa yupo nyumbani.