NBAA: Tanzania inakabiliwa na uhaba wa wahasibu 3,000

Thursday December 6 2018

Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Uhasibu na

Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), Profesa Isaya Jairo 

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa Tanzania ina uhaba wa wahasibu 3,000, lakini wapo ambao hawana ajira licha ya kuhitajika katika idara za Serikali, mashirika na kampuni.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Desemba 6, 2018 na Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA), Profesa Isaya Jairo katika mkutano wa mwaka wa bodi hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam.

"Hivi sasa tuna wahasibu takribani 6,000, lakini bado kuna mashirika na idara za Serikali zenye uhitaji wa wataalamu hao licha ya kuwa wapo ambao bado hawajapata ajira," amesema Profesa Jairo.

“Wakati huu ambapo Serikali inatekeleza mpango wake wa uchumi wa viwanda, wahasibu wanahitajika zaidi ya 3,000. Huenda wakahitajika zaidi ya hao endapo kasi ya ujenzi wa viwanda itakuwa kubwa zaidi.”

Ameongeza kuwa uchache wa wataalamu hao unatokana na uchache wa vyuo pamoja na fikra potofu kwamba kozi za uhasibu ni ngumu wakati si kweli.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Amina Shaaban amesema wahasibu na wakaguzi wa fedha ni watu muhimu katika maendeleo hususani uchumi wa viwanda.

"Wahasibu  ndiyo wanaofanya uchambuzi wa mambo ya fedha na kuandaa ripoti za hesabu za fedha za uhakika ambazo zinasaidia katika ukusanyaji wa kodi, kuimarisha uchumi na kuvutia uwekezaji," amesema Shabaan.

Amesema wahasibu na wakaguzi wa hesabu wanayo nafasi kubwa kufanikisha safari ya uchumi wa viwanda, hivyo kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kujiona kuwa ana deni kwa Taifa.

Advertisement