NBC yatoa mikopo ya Sh155 bilioni

Muktasari:

Benki ya Taifa ya biashara (NBC) imetoa mkopo ya Sh155 bilioni kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati 3000 katika kuanzia 2016 hadi Machi, 2019

Dar es Salaam. Benki ya Taifa ya biashara (NBC) imetoa mkopo ya Sh155 bilioni kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati 3000 katika kuanzia 2016 hadi Machi, 2019.

Akizungumza katika ufunguzi wa tawi jipya la Tegeta leo Julai 18,2019, kaimu mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo,  Gaudence Shawa amesema kwa kutambua umuhimu wa wafanyabiashara wadogo na wakati mwaka 2016 NBC iliunda kurugenzi maalum ya kuhudumia wateja wake.

"Kwa umuhimu wa kundi hili la wateja NBC kwa kushirikuana na shirika tanzu la benki ya Dunia imefanya mapitio  ya kina na utaratibu mzima wa utoaji mikopo kwa kundi hili,” amesema Shawa.

Amebainisha kuwa baada ya muda mfupi benki hiyo itakuwa na utaratibu ulioboreshwa wa kuwahudumia,  kuwawezesha wateja wadogo kwa maelezo kuwa wana nafasi katika kutekeleza azma ya Serikali ya kujenga Tanzania ya viwanda.

Shawa amesema benki hiyo pia inatambua wastaafu wanaopokea pensheni kama kundi lenye uwezo wa kuchangia  uchumi wa Taifa kwa kuwezeshwa kifedha.

"Sasa ipo bima inayowakinga wastaafu waliovuka umri wa miaka 60 tofauti na hapo, nyuma mikopo ilitolewa kwa wafanyakazi wenye mishahara tu,” amesisitiza.

Meneja uhusiano wa NBC,  William Kallaghe amesema benki hiyo imejiunga na mfumo wa kukusanya fedha za umma,  mwaka 2018 hadi kufikia Desemba ilikuwa imekusanya maduhuli ya Serikali ya Sh201 bilioni.