NDC yawatangazia neema wakulima, kuwakopesha matrekta kwa kutumia barua

Mkurugenzi Mwezeshaji wa Shirila la Taifa la Maendelea (NDC), Profesa Damian Gabagambi, akizungumza wakati wa Mkutano na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika Viwanja vya Jk Nyerere barabara ya Kilwa. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Ili kuondoa kilimo cha jembe la mkono na kukuza uzalishaji wa malighafi katika kuelekea uchumi wa viwanda Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) nchini Tanzania limeandaa mkakati wa kuwagusa wakulima mmojammoja kwa kuwapatia mikopo ya matrekta isiyo na riba kwa miaka miwili

Dar es Salaam. Mkurugenzi mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) nchini Tanzania, Profesa Damian Gabagambi amesema katika msimu wa maonyesho ya 43 ya sabasaba wameandaa mkakati maalumu wa kuwakopesha wakulima wa vijijini matrekta kwa kutumia barua.

Amesema barua hiyo ya maombi inapaswa kutoka kwa ofisa mtendaji wa kata kupitia kwa Ofisa Mtendaji wa Kijiji na Mkurugenzi wa halmashauri anayotoka.

Amesema hatua hiyo imefikiwa ili kupunguza matumizi ya jembe la mkono na kuendana na kasi ya uchumi wa viwanda kwa kumgusa mkulima mmojammoja.

Maonyesho ya 43 ya biashara ya kimataifa yalianza rasmi Juni 28, 2019 na yanatarajiwa kukamilika Julai 13, 2019 huku yakishirikisha zaidi ya nchi 35.

Akizungumza na waandishi wa  habari katika maonyesho hayo leo Jumatatu Julai 1, 2019, Profesa Gabagambi amesema mkulima huyo ataweza kulipia mkopo wake kwa miaka miwili bila riba tangu kukopa kwake.

“Inategemea na aina ya trekta analohitaji na akija na vielelezo hivyo atalipia Sh3 milioni na kupewa trekta lake lakini kama atashindwa kulipa ndani ya muda wa makubaliano ataanza kutozwa riba baada ya miaka miwili na tunapitia kwa viongozi hao kwa sababu wao wanawafahamu,” amesema Profesa Gabagambi

“Tunataka jembe la mkono tuliweke makumbusho ya taifa kwa sababu kasi ya uzalishaji wa malighafi inayohitajika sasa ni ile itakayoendana na viwanda vyetu pamoja na kuhudumia viwanda vya nchi jirani hivyo kwa jembe hatutaweza kufika mbali,” amesema