NEC: Tutafuata uamuzi wa mahakama uchaguzi mkuu

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage akizungumza wakati wa Mkutano na wahariri uliofanyika jijini, Dar es Salam leo. Kulia ni Mkurugenzi wa Tume hiyo, Athuman Kihamia. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Tume ya Uchaguzi yaweka wazi kutowatumia wakurugenzi kwenye usimamizi wa uchaguzi kama ilivyoelekezwa na mahakama


Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imeweka wazi kuwa vifungu vya sheria ya uchaguzi vilivyolalamikiwa na kutenguliwa na mahakama havitatumika kwenye utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo.

Vifungu hivyo ni kifungu cha 7(1) na 7(3) vinavyowapa mamlaka wakurugenzi wa halmashauri kama wasimamizi wa uchaguzi. Vifungu hivyo vinawataja wakurugenzi wa jiji, wakurugenzi wa manispaa, wakurugenzi wa miji na wakurugenzi wa wilaya (DED) kwamba wanaweza kuteuliwa na tume kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Akizungumza wakati wa mkutano na wahariri wa vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Nec Jaji Semistocles Kaijage alisema wanazingatia maelekezo ya mahakama hivyo Nec haitotumia vifungu hivyo vilivyolalamikiwa.

Jaji Kaijage aliyasema hayo wakati akijibu swali la mhariri wa gazeti la The Citizen Damas Kanyabwoya aliyetaka kufahamu kama Nec itaendelea kuwatumia wakurugenzi baada ya uamuzi wa mahakama.

“Mahaka ilitimiza wajibu wake ikavitengua baadhi ya vifungu vya sheria vilivyolalamikiwa. Niwahakikishie kuwa vile vifungu vilivyolalamikiwa hatutavitumia katika utekelezaji wa majukumu yetu. Kifungu cha 7 (1) na 7(3) cha sheria ya taifa ya uchaguzi ndivyo vilivyotenguliwa, vingine havijalalamikiwa,”