NMB ilivyosheherekea siku ya wanawake

Mkurugenzi mwendeshaji kutoka Mfuko wa Kuendeleza Huduma za Fedha (FSDT) Bi. Irene Madeje  Mlola  (kulia)   wakati wa mdahalo uliondaliwa na benki ya NMB ikiwa ni maadhimishi ya siku ya wanawake Duniani. Kushoto ni Afisa Mkakati na Uwekezaji wa NMB Caroline Yambesi  na Mkurugenzi wa Trademark East Africa tawi la Tanzania Bw. John Ulanga (katikati).

Dar es Salaam. Wanaume wana nafasi kubwa katika kufanikisha uwepo wa usawa wa kijinsia kwenye jamii kuanzia ngazi ya familia na hata katika maeneo ya kazini.

Katika kufanikisha hilo, wanaume hawana budi kubadili mtizamo hususan wa masuala yahusuyo wanawake, jambo ambalo litatengeneza mazingira mazuri katika kuchagiza usawa wa kijinsia kwenye jamii.

Mtazamo huo umeelezwa na wadau wa masuala ya jinsia na maendeleo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati mjadala  ulioandaliwa na benki ya NMB ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani mwaka huu iliyobeba ujumbe wa “#balanceForBetter”.

Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu wa NMB, Emmanuel Akonaay, amesema mara nyingi wanawake wamekuwa wakionekana hawawezi kuzalisha mali kwa ufanisi zaidi katika kampuni au shirika ikilinganisha na uwezo walionao mwanaume.

“Mitazamo kama hii haina budi kubadilika. Kwani baadhi ya mabosi wamekuwa wakifikiri kuwa uwezo wa uzalishaji mali unapungua pale mwanamke anaposhika tu ujauzito hadi wakati wa likizo ya uzazi,” ameeleza.

Kwa maoni yake, Akonaay amesema usawa wa kijinsia hautoweza kufikiwa kwa kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za uongozi pekee bali kwa ushirikishwaji wao na kutoa usawa katika nafasi hizo kwa kuzingatia vigezo vya kitaaluma.  

Akichangia mada katika mjadala huo, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Kuendeleza Huduma za fedha (FSDT) Irene Mlola amesema kwa upande mwingine uwepo wa idadi isiyo sawa ya ushirikishwaji na ujumuisho wa wanawake katika masuala ya kifedha ikilinganishwa na upande wa wanaume ni dhahiri unaonesha kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia.

Naye John Ulanga , Mkurugenzi mkaazi wa Trademark East Africa, amesema ni vyema kila kiongozi  kuboresha mazingira ya kazi kwa kila mfanyakazi na kuwa kila mmoja mwanamke na mwanaume ni muhimu kubadili mitazamo yao kuhusiana na usawa baina ya mwanamke na mwanaume.

Caroline Yambesi ambaye ni Afisa Mkakati na Uwekezaji wa Benki ya NMB amesema ni wakati muafaka wa kutengeneza mazingira chanya ambayo yatamruhusu mwanamke kuwa huru kufanya kazi zake kama mama na kuwa kama kiongozi kazini.