UCHOKOZI WA EDO:Nadhani picha ya Komredi Polepole mkutanoni ni ‘photoshop’

Jana nilivaa miwani, nikavua, nikavaa tena. Sikuamini nilichokiona. Nikamwita kijana mdogo mwenye macho yenye afya zaidi anisomee maandishi ya chini ya picha ya komredi Polepole. Ilitoka katika ukurasa wa 3 wa gazeti hili toleo la jana.

Picha ilimuonyesha komredi Polepole akiwa katika mkutano wa hadhara pale Karatu akihutubia wananchi katika kivazi maridadi cha chama chake. Mpaka sasa nadhani kuna makosa ya kiuandishi chini ya ile picha. Naamini Namba Moja bado hajaruhusu mikutano ya hadhara.

Namba Moja ameruhusu mikutano ya kisiasa ya wabunge katika maeneo yao. Majuzi tu alikutana na swali korofi la kiongozi mmoja wa dini aliyetaka watu waruhusiwe kufanya siasa zao. Akamjibu kwa ufafanuzi mzuri kwamba mikutano ya siasa ipo kwa ajili ya wabunge katika maeneo yao.

Naamini picha ya Polepole huenda ni ya ‘photoshop’. Tunapozungumza photoshop tunazungumzia ile tabia ya vijana wa kisasa kutengeneza picha na kuziunganisha katika matukio ambayo hayana uhusiano.

Siamini kama komredi Polepole anaweza kuvunja amri ya Namba Moja kiurahisi. Wakati huu ambao Namba Moja ametoka kusisitiza haki na kuijenga jamii iliyo sawa siamini kama upande mmoja unaweza kuruhusiwa kufanya mikutano halafu mwingine uzuiwe.

Nategemea komredi Polepole atakuja juu kwa picha yake kutengenezwa akiwa katika mkutano wa siasa kinyume na amri ya Namba Moja au kama ni kweli alikuwa ni yeye katika ule mkutano basi anaweza kumuomba radhi Namba Moja kwa kuvunja amri yake.

Siamini pia kama Polisi wanaweza kumuacha ahutubie wakati imekuwa ikiwakamata wanasiasa wengine hasa wale wa upinzani ambao wamekuwa wakihutubia mikutano ya hadhara.

Hapa ndipo ninapojaribu kujiaminisha kwamba ile picha ya komredi Polepole inaweza kuwa ni photoshop.

Nategemea ataitolea maelezo muda mchache ujao. Siku hizi nchi yetu inaongoza kwa kuwa na watu wa kada mbalimbali wanaopenda kufanya mikutano na waandishi wa habari bila ya sababu za msingi. Nadhani mkutano wa waandishi wa habari na komredi Polepole utakuwa wa msingi sana. Nausubiri kwa hamu.