Nafasi ya Profesa Majimarefu yajazwa CCM

Muktasari:

  • Nafasi ya ujumbe wa baraza kuu la wazazi wa CCM iliyokuwa ikishikiliwa na Profesa Majimarefu, imepata mrithi

Dodoma. Nafasi ya ujumbe wa baraza kuu la wazazi CCM iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani maarufu ‘Profesa Majimarefu’ imepata mrithi.

Jana usiku Jumatatu Januari 7, 2019 baraza hilo lilimtangaza Rajabu Mwilima kuziba nafasi ya Profesa Majimarefu aliyefariki dunia Julai 2, 2018 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katibu wa jumuiya ya wazazi, Erasto Sima alisema Mwilima aliwashinda wenzake watatu na kuibuka katika nafasi hiyo ambayo kwao ilikuwa ni muhimu ijazwe.

Sima amesema katika uhai wake Profesa Majimarefu alikuwa kiungo muhimu sana kwenye jumuiya na michango yake itaendelea kukumbukwa.

Baraza pia lilimchagua Galila Wabanhu kuziba nafasi ya ujumbe wa halmashauri kuu ya CCM iliyoachwa wazi na Kitwana Komanya ambaye aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Tabora

Wakati huo huo, katibu ameutaja mkoa wa Mwanza kwamba unaongoza kwa kusajili wanachama wengi huku mkoa wa Kusini Unguja ukiwa wa mwisho.

"Hadi sasa Mwanza imesajili wanachama 15,486 wakati Kusini Unguja wamesajili wanachama tisa jambo amba linaonyesha kuwa bado kuna kazi inatakiwa kufanywa," alisema.

Mwenyekiti wa umoja huo, Dk Edmund Mndolwa amewataka wanajumuiya kupambana kwa nguvu zote ili kufanikisha ushindi wa CCM na kumrudisha madarakani 2020.

Dk Mndolwa amewaagiza wajumbe kutokulala kama ilivyo kwa wapinzani ambao wameishiwa sera na hawawezi kushinda hata uchaguzi wa Serikali za mitaa.