Nafasi za uongozi TPDC zashtua kamati ya bunge

Saturday March 16 2019

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kapuulya Musomba 

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imesikitishwa na viongozi wengi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kukaimu nafasi zao kwa muda mrefu, jambo ambalo linapunguza utendaji kazi.

Jana kamati hiyo ilitembelea mitambo ya gesi ya Kinyerezi jijini Dar es Salaam na wakati wa utambulisho wa viongozi wa shirika hilo, wengi walibainika kuwa wanakaimu nafasi zao kwa miaka mitatu sasa.

Nafasi zinazokaimiwa ni pamoja na mkurugenzi mkuu, mkurugenzi wa mkondo wa juu, mkurugenzi wa mkondo wa chini, wakurugenzi wa kampuni tanzu za Tanoil na Gasco, mkuu wa kitengo cha usimamizi wa hatari na mkuu wa kitengo cha manunuzi.

Akizungumzia suala hilo, mwenyekiti wa kamati ya PIC, Raphael Chegeni aliiagiza bodi ya TPDC kuchukua hatua za haraka kujaza nafasi zote zinazokaimiwa ili watendaji husika wawe na nguvu ya kufanya maamuzi katika nafasi zao.

“Watendaji wengi wanakaimu nafasi zao kwa muda mrefu, kwanini wasithibitishwe kama wanafanya vizuri? Bodi chukueni hatua kujaza nafasi zinazokaimiwa na mtuletee ripoti baada ya kufanya hivyo,” aliagiza Chegeni.

Awali, akizungumzia suala hilo, mwenyekiti wa bodi ya TPDC, Jaji mstaafu Josephat Makanja alisema viongozi hao wanakaimu nafasi zao kwa sababu mbili; kwanza wapo wanaokaimu nafasi za watendaji ambao wana kesi za jinai mahakamani na pili wapo wanaokaimu kwa sababu ya mabadiliko ya kimuundo katika shirika hilo.

“Tulitoa mapendekezo kwa katibu mkuu kiongozi ya mabadiliko ya muundo wa shirika na yameridhiwa, sasa tutaanza kujaza nafasi hizo. Kwa nafasi ya mkurugenzi mkuu hilo siwezi kuzungumzia kwa sababu hiyo ni mamlaka ya uteuzi wa Rais na Rais anajua nini cha kufanya,” alisema.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa bodi alisema watendaji hao wamekuwa wakifanya kazi vizuri bila kujali kwamba wanakaimu nafasi zao ndiyo maana shirika hilo linakwenda vizuri katika kutekeleza majukumu yake.

Alisema mpaka sasa shirika hilo linaongozwa kwa asilimia 100 na Watanzania wenyewe na kwamba wataalamu waliokuwapo siku za nyuma wote wameondoka na kuwaacha wazawa.

Advertisement