Naibu Kaadhi mkuu wa Zanzibar ahimiza wenye nacho kuwasaidia wengine

Naibu Kaadhi mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali

Muktasari:

Wakati zikiwa zimesalia siku takribani kumi kufikia sikukuu ya Eid el Fitri, Waumini wa dini ya kiisalimu wenye uwezo visiwani Zanzibar wametakiwa kutoa zaka zao kwa lengo la kuwafariji wasiokua na uwezo.

Unguja. Naibu Kaadhi mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali amesema katika kipindi cha kuelekea sikukuu ya Eid el Fitri ni vyema kwa wenye uwezo kujitoa kuwasaidia wengine wasiokua nacho.

Sheikh Ngwali ameyasema hayo leo Mei 26 mwaka 2019, Wakati akizungumza na waumini mbalimbali wa dini ya Kiislam wakati wa uzinduzi wa mfuko wa zaka wa jumuia ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA)

Amesema iwapo wananchi wenye uwezo watajitoa kuwasaidia wengine ni sawa na kutakasa mali zao na kuzifanya zenye baraka zaidi.

Ameongeza kuwa katika maeneo mbali visiwani Zanzibar wapo watu wasiokua na uwezo ambao wanahitaji kusaidiwa hivyo ni vyema watu kujitoa na kuchangia zaka yao kwa ajili ya watu hao.

Hata hivyo Sheikh Hassan amewatoa hofu wale wote wenye wasiwasi na kutoa mali zao kwamba kila watakachokitoa kitawafikia walengwa na si vinginevyo.

“Huenda ikawa wapo baadhi ya watu wenye uwezo wanahofia kufikisha zaka yao haitofika kwa walengwa lakini kupitia taasisi hii nina hakika hilo halitafanyika,” amesema