Naibu Waziri ataka wananchi kuvuna maji ya mvua

Muktasari:

Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso amewataka wananchi kuvuna maji ya mvua ili kujihakikishia usalama wa maji kwenye makazi yao. Amesema Serikali pia inatekeleza miradi mikubwa ambayo itavuna maji ya mvua na kusambaza kwa wananchi.

Dar es Salaam. Wakati mataifa mbalimbali yakiadhimisha Siku ya Maji duniani, Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewataka wananchi kuvuna maji ya mvua na kutumia fursa hiyo kujihakikishia usalama wa maji kwenye kaya zao.

Aweso amesema tayari Serikali imechukua hatua ya ujenzi wa mabwawa ya kuvuna maji ya mvua akitolea mfano Bwawa la Kidete lililoko Kilosa ambalo litakuwa likivuna maji ya mvua katika eneo la Kilosa ambalo limekuwa likiathiriwa na mafuriko.

Akizungumza katika kilele cha Wiki ya Maji leo Ijumaa Machi 22, 2019 jijini Dar es Salaam, Aweso amesema Tanzania ina miradi mbalimbali ya maji kutoka vyanzo mbalimbali, lengo likiwa ni kuwapatia maji Watanzania hasa vijijini kwa umbali usiozidi mita 400.

“Kila Mtanzania atengeneze miundombinu ya kuvuna maji nyumbani kwake ili ukame unapotokea basi anakuwa na akiba ya kutosha kwa matumizi yake. Kitaifa, Serikali pia ina mipango hiyo,” amesema Aweso.

Naibu Waziri huyo amesema anajua wananchi wengi wanahitaji kuunganishiwa maji, hivyo ameziagiza mamlaka za maji kote nchini ziweke utaratibu wa kuwaunganishia maji na kuwakata fedha kidogo kidogo.

Amewaonya pia watendaji wa mamlaka hizo ambao wanawaongezea wateja bili za maji kwamba kitendo hicho ni ukosefu wa maadili ya kazi. Ili kupambana na hali hiyo, Aweso amesema Serikali imeanzisha mfumo wa pre-pay ambao utamwezesha mteja kulipia maji kwa kiwango alichotumia.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa uzalishaji na usambazaji maji kutoka Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (Dawasa), Aron Joseph amesema katika wiki ya maji wamewasikiliza wateja 150 ambao wengi wao wamelalamikia kero kubwa ya kuongezewa bili ya maji.

“Tumepokea kero 150, nyingi tumezitatua hapa hapa lakini nyingine 30 tunaendelea nazo kwa sababu utatuzi wake unachukua muda kidogo. Kwa ujumla tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi juu ya huduma zetu hasa mifumo ya malipo ya maji,” amesema Joseph.