Naibu Waziri atoa siku 90 waliovamia hifadhi kuondoka

Muktasari:

Naibu waziri wa maliasili na utalii, Constantine Kanyasu ametembelea shamba la misitu lililopo ndani ya msitu wa hifadhi wa Biharamulo mkoani Kagera na kuagiza wananchi waliovamia shamba hilo kuondoka ndani ya kipindi cha miezi mitatu (siku 90)

Chato. Naibu waziri wa maliasili na utalii, Constantine Kanyasu ametoa siku 90 kwa wakulima waliovamia eneo la shamba la misitu lililopo ndani ya msitu wa hifadhi wa Biharamulo mkoani Kagera kuondoka katika maeneo hayo la sivyo watakaoendelea kukaidi watakamatwa kwa mujibu wa sheria.

Mbali na kutoa siku 30 kwa wakulima, ametoa wiki mbili kwa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Chato kufanya operesheni ya kuwaondoa wafugaji waliovamia shamba hilo na kulisha mifugo miti iliyopandwa.

Akizungumza wakati alipotembelea shamba hilo jana Alhamisi Machi 22, 2019, Kanyasu alisema pamoja na tamko la Rais John Magufuli la kutaka wizara kurasimisha vijiji vilivyoko karibu na hifadhi, wananchi wamevamia maeneo kabla ya kuruhusiwa na kufanya uharibifu mkubwa.

"Naomba muwaeleze wananchi wenu kama wataendelea kuingilia maeneo kabla kamati haijamaliza kazi tutawakamata, watumishi wetu wanapigwa na mnafanya uharibifu mkubwa hatutavumilia," alisema.

Kanyasu alisema maombi yanayotumwa na Serikali za wilaya, mkoa na vijiji vimeongezeka kutoka 366 hadi zaidi ya 700 na kwamba kamati ilipewa mwezi mmoja na sasa imeomba kuongezewa mwezi mwingine ili waweze kuchagua vijiji vya kurasimishwa kwa kuwa si vyote vyenye sifa.

Akizungumzia kadhia wanazokutana nazo watumishi kutokana na uvamizi wa maeneo ya hifadhi, Kanyasu alisema kwa mwaka huu watumishi 10 wameuawa na wanaovamia wakiwa na silaha na kusema Serikali haitaendelea kuvumilia hali hiyo.

Meneja wa shamba la miti Biharamlo, Thadeus Shirima alisema watumishi wamekuwa wakivamiwa na kupigwa na wananchi wanaovamia maeneo hayo kwa madai kuwa Rais aliruhusu wananchi kuingia hifadhini.