Nancy Lema: Msomi mwenye ‘Master’ anayejivunia kuuza makande

Mwanza. “Elimu ni ufunguo wa maisha” Huu ni usemi wa wahenga uliozoeleka na hutumiwa kuhimiza suala la elimu.

Usemi huu unamaanisha kuwa mwenye elimu ana fursa na uwezo zaidi kufikiri na kupata mbinu za kutumia mazingira na nyenzo zinazomzunguka kukabiliana na changamoto za maisha.

Hata kwa nafasi za ajira, mwenye elimu na ujuzi hupewa nafasi ya kwanza katika ajira rasmi zenye kipato na maslahi mazuri.

Vijana wengi wenye elimu ya kiwango cha shahada, uzamili na uzamivu hutarajia kupata ajira zinazolipa kwenye ofisi nzuri, kubwa na zenye kila aina ya maslahi.

Wengi wa wenye fikra hizi huzunguka kutwa kwenye ofisi mbalimbali kutafuta ajira, mikononi mwao wakiwa na bahasha za kaki zenye vyeti, barua za kuomba kazi na maelezo binafsi.

Nancy Lema (29) ni kati ya vijana wa Kitanzania waliopata fursa ya kupata elimu ya juu ndani na nje ya nchi ambaye alitarajia kupata ajira nzuri inayolipa katika sekta rasmi.

Baada ya kuhitimu shahada yake ya uzamili nchini Marekani na kureja nchini, Nancy alitafuta kazi nzuri inayolipa kulingana na elimu yake lakini hakufanikiwa kuipata.

Hapo ndipo wazo la kutumia elimu yake kujiajiri na kutengeneza ajira kwa wengine lilipomjia.

Unajua msomi huyu, mkazi wa mtaa wa Capri-Point jijini Mwanza, aliwaza kujiajiri na kutengeneza ajira kupitia shughuli gani?

Baada ya kufanya utafiti wa kina na kubaini wateja na mahitaji yao, Nancy alianzisha biashara ya kupika na kuuza vyakula vya asili, yakiwamo makande.

Nancy aliyepata shahada ya kwanza ya masuala ya fedha kutoka Chuo cha St Cloud State nchini Marekani, mwaka 2013, anapika na kuuza makande.

Pamoja na makande, pia anapika na kuuza aina nyingine ya vyakula kama wali, ugali, chapati, pilau, biriani, ndizi mshale na matoke, tambi, samaki, nyama ya ng’ombe, kuku, kisamvu, maharagwe, njegere, bamia na matembele. Pia anatengeneza saladi maalumu kwa wanaohitaji kupunguza uzito wa miili yao pamoja na vyakula vya kuchemsha na ‘brown rice’ isiyo na wanga kama ilivyo wali mweupe.

Alifikiriaje biashara hii?

“Baada ya kurejea nchini kutoka Marekani, nilijitahidi kutafuta kazi sehemu mbalimbali bila mafanikio. Akili ya kuanzisha biashara ikanijia lakini swali likawa ni biashara gani nitaifanya kwa ufanisi na faida?” anasimulia Nancy na kuongeza, “nilifanya utafiti na kubaini kuwa biashara inayolipa jijini Mwanza na maeneo mengine ya mijini ni kupika na kuuza vyakula.”

Anasema alianza kupika kwa majaribio, siku ya kwanza alipika akiwa nyumbani na kuwagawia chakula cha bure ndugu, jamaa na marafiki zake katika ofisi mbalimbali.

Wakati akiendelea kupika na kugawa chakula bure kwa watu kama njia ya kujitangaza na kupata soko, anasema aliendelea kufanya utafiti wa aina gani ya chakula cha kumwezesha kukamata na kumiliki soko.

“Nilibaini wengi wa wanaofanya biashara ya kupika na kuuza vyakula hapa jijini wamejikita kuuza vile vya kisasa vilivyozoeleka. Hapa nikaona fursa ya vyakula vya asili; ndipo nikafikiria kupika na kuuza makande,” anasema.

Anasema alichagua makande kwa sababu ni chakula kinacholiwa na makundi yote ya watu kuanzia wenye uwezo wa juu, kati na chini.

“Asilimia kubwa ya Watanzania wamezaliwa na kukulia vijijini ambako makande ni kati ya vyakula vikuu. Lakini baada ya kuja mijini aidha hawapati fursa ya kupika na kupikiwa makande licha ya ukweli kwamba ni chakula kilichowakuza wengi,” anasema Nancy.

Msomi huyu aliyepata elimu yake ya awali Shule ya Msingi Nyakahoja jijini Mwanza alikohitimu mwaka 2006 kabla ya kujiunga International School of Moshi kwa elimu ya sekondari na kuhitimu mwaka 2012, anasema licha ya ladha tamu mdomoni, makande pia huongeza virutubisho kadhaa mwilini ikiwemo wanga na protini.

“Wengi hudhani makande kinaliwa na watu waishio vijijini wasiojiweza, dhana ambayo siyo sahihi,” anasema Nancy.

Kwa yeyote ambaye ni mkazi au amewahi kufika eneo la Capri-point jijini Mwanza jina la “Up Town Kitchen” haliwezi kuwa geni kwake. Hili ni eneo maarufu kutokana na aina ya chakula kinachopatikana hapo. Makande ya Nancy!

Ingawa wateja wengi wanahudumiwa kwa kufikishiwa mahitaji mahali walipo, baadhi yao hufuata huduma hiyo hapo hapo Up Town Kitchen.

“Wafanyakazi wa mabenki mbalimbali, ofisi binafsi pamoja na zile za umma, mafundi magari, waendesha bodaboda na madereva taxi ni miongoni mwa wateja wetu wakuu tunaowafikishia huduma pale walipo.

“Kuna namba tunazozitangaza kupitia mitandao ya Facebook, Instagram na WhatsApp, mteja akitupigia simu tunamfikishia huduma mahali alipo kwa malipo ya Sh5,000 inayojumuisha gharama ya chakula na usafiri,” anasema Nancy.

Anasema kwamba kwa siku hupokea oda ya zaidi ya sahani 40 za chakula. Kila sahani moja inauzwa kwa bei ya Sh5,000 kwa mteja anayepelekewa mahali alipo, lakini kwa wateja wanaofika Up Town Kitchen huuziwa kwa bei ya Sh3,000.

Ili kurahisisha mawasiliano kati ya anayeandaa chakula na mpokea oda za wateja, Nancy hutumia mawasiliano ya radio ya upepo, mazungumzo ya anayepokea oda husika huwafikia moja kwa moja wapishi na wanaoandaa vyakula vya kwenda kwa wateja wake wa nje.

Anachojivunia Nancy

“Pamoja na kupata ajira ya uhakika na kutengeneza ajira kwa watu wengine, kazi hii pia imenipa mafanikio makubwa kimaisha kwa kuniwezesha kuwatunza wazazi wangu pamoja na kuwasomesha wadogo zangu,” anasema Nancy kwa kujiamini.

Up Town Kitchen imetoa nafasi 12 za ajira za kudumu na za muda kwa vijana katika nafasi za upishi, usafi, kupokea oda na kusambaza vyakula kwa wateja.

“Pia nimeweza kujenga na kupata marafiki wengi. Wapo niliokutana nao kupitia kurasa za mitandao ya kijamii na wengine ofisini. Baadhi ya hawa huomba na kupata ushauri kwangu jinsi ya kuanzisha na kuendesha biashara kwa ufanisi,” anasema Nancy.

“Usomi siyo vyeti; bali ni matokeo chanya yanayopatikana katika jamii yako kupitia elimu yako. Najivunia kupata fursa ya kuisaidia jamii yangu kwa kiwango hiki ninachoweza,” anajisifia Nancy huku akiahidi kuongeza juhudi, maarifa na ubunifu zaidi katika kazi yake.

Changamoto

Anasema changamoto ni za kawaida, anasema baadhi ya watu kumwangalia na kumfikiria tofauti kwa kuangalia kiwango chake cha elimu na shughuli anayoifanya.

“Mara nyingi wanaonishangaa kwa kupika na kuuza makande badala ya kutafuta ajira, nawasisitizia kuwa jambo muhimu ni kipato cha uhakika kwa njia halali. Huwa nawakumbusha usemi wa wahenga wa bora mkono uende kinywani.”

Msomi huyo anakusudia kuboresha ladha, ubora na usalama wa chakula na hatimaye kupata hati ya ubora kutoka taasisi zinazosimamia ubora wa vyakula nchini.