VIDEO: Nape adai korosho ipo ICU, amtaja CAG

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya kilimo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Mbunge wa Mtama (CCM),  Nape  Nnauye amesema zao la korosho liko chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) na kutaka mkakati wa ununuzi wa zao hilo kupitiwa kwa makini

Dodoma. Mbunge wa Mtama (CCM),  Nape  Nnauye amesema zao la korosho liko chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) na kutaka mkakati wa ununuzi wa zao hilo kupitiwa kwa makini.

Waziri huyo wa zamani wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Mei 20, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka 2019/2020 na kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua udanganyifu wa mauzo ya korosho.

Amesema waliohusika kwenye udanganyifu wa mauzo ya korosho wawajibike wenyewe vinginevyo atapeleka kusudio la namna ya kuwawajibisha.

Amesema baada ya ukaguzi huo wa CAG taarifa ipelekwe bungeni ijadiliwe kwa maelezo kuwa kinachoelezwa kuhusu ununuzi wa korosho ni uongo.

"Nia ya Rais ilikuwa njema kabisa  lakini waliokwenda huko wamefanya mazonge na mambo ya hovyo, hapa tukubaliane siyo Serikali yote imeharibu bali wako waliofanya mambo ya hovyo,  ni vema wakawajibika ama kuwajibishwa," amesema Nape.

Mbunge huo amesema waziri wa Kilimo na naibu wake hawahusiki katika sakata la korosho, kwamba wapo wanaotakiwa kuwajibika.

Mbunge huyo amesema uchunguzi utakaofanyika pia uangalie ubora wa korosho kwa madai kuwa zikikaa zaidi ya miezi sita haziwezi kuwa salama.

Nape ametoa mfano jimboni kwake kwamba kuna vyama vya ushirika 11 na wakulima 1,281 lakini hakuna aliyelipwa licha ya taarifa kueleza kuwa wamelipwa.

Mbunge huyo ameitaka Serikali kupeleka bungeni sheria ya korosho ifumuliwe kwa kuwa imekuwa chungu kwa wakulima wa zao hilo.