UCHOKOZI WA EDO: Nape ananikumbusha hadithi ya zamani ya mmakonde na mshale

Nape Nnauye. Mtoto wa marehemu Mzee Moses Nnauye ambaye alikuwa rafiki wa baba yangu Marehemu Mzee John Kumwembe. Tuseme wote ni marehemu kwa sasa. Mzee Nnauye alikuwa rafiki wa Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa anakijua vyema chama.

Wakati ule Nape akichomoza kama kijana katika chama sikujua kama na yeye angekuwa na nguvu kama alizo nazo sasa, eti na yeye angekuwa mtu anayekijua sana chama. Hata hivyo, nyakati zinakwenda kasi. Leo yeye ni kama baba yake tu wa enzi hizi.

Majuzi akanikumbusha wamakonde wa zamani wale waliokuwa walinzi. Siku hizi walinzi ni wamasai na mbwa, zamani walikuwa wamakonde. Walikuwa waaminifu na wenye roho za korosho.

Ukiwa katika harakati za kuiba mmakonde anavuta mshale wake anakwambia “ukisimama nchale, ukikimbia nchale, ukikaa nchale, ukiongea nchale, ukikaa kimya nchale”. Sijui wale wamakonde walitaka mwizi afanye nini zaidi?.

Majuzi Nape aliachana na uenyekiti wa kamati ya ardhi. Tukaguna. siku moja baadaye akaposti picha ya saa tu katika mtandao wake wa Twitter tukaguna. kila analofanya siku hizi watu wanaguna. Akiongea wanaguna, akikaa kimya wanaguna, akiposti hata anakunywa chai watu wanaguna.

Yeye na yule baba yake aliyemuachia jimbo wanawafanya wambea wa kisiasa waishi na kihoro. Wakikaa kimya kwetu ni habari. Wakiongea kwetu ni habari. Nape hata akiweka nukta nne tu mfululizo bila ya kuandika chochote bado tunahisi kuna chochote.

Nadhani haya ni matokeo ya siasa za ukimya. Siasa za ukimya zinaleta hisia kali kuliko siasa za kuongea. Nadhani siasa za kuongea zilikuwa bora zaidi. Watu tulikuwa hatuna muda wa kudadisi. Tulikuwa tunajadili kauli tu.

Leo tunakaa tunahisi tu. Nape akikaa sana kimya, tunajiuliza, ‘hivi anajiandaa kwa jambo gani?’. Ukiamua kuwaza kwa kumuunganisha yeye na yule baba yake huwa tunajiuliza, ‘hivi wanajiandaa na jambo gani? mbona wapo kimya sana?’.

Mwaka huu wa 2019 nadhani tutahisi zaidi. Mwakani mwanzoni tutahisi zaidi. Hatuna tunachoweza kufanya. Hizi siasa za kukaa kimya ndani na nje ya chama zinawafanya baadhi ya watu kuonekana ni hatari sana na wenye mipango mingi, hata kama hawana mipango yoyote. Nadhani nimeeleweka.