Nape ataka Tanesco kugawanywa

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye akichangia mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2019/2020 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Waziri wa zamani wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema ipo haja ya kuligawa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ili kufanya kazi kwa ufanisi katika uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa nishati hiyo.

Dodoma. Unaweza kusema mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ameungana ‘kiaina’ na  mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni yaliyotolewa jana Jumanne Mei 28, 2019 kutaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kugawanywa.

Akizungumza leo katika mjadala wa bajeti ya Nishati mwaka 2019/2020 bungeni jijini Dodoma leo Jumatano Mei 29, 2019, waziri huyo wa zamani wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema licha ya jitihada zinazofanywa na wizara hiyo, kuna umuhimu wa kuligawa shirika hilo.

“Fikilieni tuigawe Tanesco kwa maana ya uzalishaji, usambazaji na uuzaji yawe yanajitegemea na upande wa uzalishaji ni vizuri tukavutia wawekezaji wa sekta binafsi wakazalisha na kusambaza,” amesema Nape.

Jana, msemaji wa  Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Nishati, John Mnyika akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu wizara hiyo amesema wamekuwa wakipendekeza mikakati mingi ya kulinusuru shirika hilo kama ambavyo nchi nyingine duniani zinafanya na moja ya mapendekezo ni kuligawanya shirika hilo.

Katika mchango wake, Nape amempongeza Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani na naibu wake, Subira Mgalu jinsi wanavyotekeleza majukumu yao ya kila siku ikiwa ni pamoja na kusimamia Wakala wa Umeme Mijini na Vijijini (Rea).

Bajeti ya Wizara ya Nishati ni Sh2.14 trilioni.