VIDEO: Nape ataka chuo cha Mwalimu Nyerere kisiwe chuo kikuu

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye akiuliza swali bungeni katika kikao cha tisa cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Nape ataka chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kisipandishwe hadhi na kuwa chuo kikuu badala yake kiboreshwe na kuwafundisha viongozi kujua wajibu wao

Dodoma. Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ameitaka Serikali kuacha kukipandisha hadhi Chuo cha Mwalimu Nyerere kuwa chuo kikuu badala yake kirudi katika msingi wake wa awali wa kufundisha mambo ya uongozi.

Nape ametoa kauli hiyo leo alipouliza swali la nyongeza kuhusu chuo hicho ambacho amesema alisoma hapo.

"Mheshimiwa mwenyekiti, mimi ni product (zao) ya Kivukoni, sikubaliani na wazo la kukipandisha hadhi chuo hicho, lengo la chuo lilikuwa ni kufundisha viongozi, je Serikali haioni umuhimu wa kukirudisha katika hali yake ili tufundishe viongozi ambao tunaona kuna haja hiyo," amehoji Nape.

Katika swali la msingi Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali ametaka kujua ni kwa nini Serikali isikipandishe hadhi chuo hicho kuwa chuo kikuu.

Bobali pia ameuliza ni kwa nini Serikali isipeleke fedha za maendeleo katika chuo hicho kama zinavyopangwa.

Akijibu, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Mwita Waitara amesema mpango wa Serikali kwa sasa si kupandisha hadhi vyuo vilivyopo bali ni kuboresha mazingira ya vyuo hivyo kwa kukarabati na kujenga miundombinu.

Kuhusu fedha, amesema Serikali imekuwa ikipeleka fedha za maendeleo katika chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kadri zinavyopatikana.

Amesema katika mwaka wa fedha 2017/18 serikali ilitoa Sh 1.2 bilioni ambazo zilitumika kukamilisha ujenzi wa hosteli ya wanafunzi.