Nchi maskini duniani zashauriwa kuwakwamua wajasiriamali

Thursday November 22 2018

By Kelvin Matandiko Mwananchi [email protected]

Dar es salaam. Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo na Biashara (UNCTAD), imezishauri nchi maskini duniani ikiwamo Tanzania kuweka mazingira mazuri ya biashara yatakayoibua na kuendeleza wajasiriamali wadogo.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Novemba 22, 2018 jijini Dar es Salaam na ofisa mchumi wa UNCTAD, Dk Benjamin  Banda wakati akiwasilisha ripoti ya kamati hiyo ya ‘Mchango wa ujasiriamali katika kuleta mabadiliko endelevu ya 2018’.

Dk Banda ambaye ni miongoni mwa watafiti wa ripoti hiyo, amesema njia pekee kwa nchi katika kusaidia wajasiriamali wake ni kuongeza thamani ya bidhaa, kurasimisha bidhaa, kutoa mikopo yenye riba nafuu na kutoa semina za ujasiriamali ili kuongeza ubunifu, wabunifu utakaohimili ushindani wa soko la Afrika na duniani.

UNCTAD hufanya tafiti zenye dhima mbalimbali kila mwaka zinazojikita katika mbinu za kukwamua wajasiriamali waliopo kwenye nchi maskini duniani.

Ripoti hiyo ya dunia kwa mwaka 2018 imetumia nchi 47 ikiwamo Tanzania, ikichambua changamoto wanazokutana nazo wajasiriamali wa nchi hizo na kushauri hatua zinazohitajika ili kuwa na mchango katika maendeleo endelevu ya nchi husika.

Dk Banda amesema fursa za masoko ni nyingi katika nchi zilizoendelea, hivyo Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi kwa nchi hizo wanatakiwa kujipanga ili kuzitumia.

Utafiti huo uliofanyika kati ya Novemba 2017 hadi Novemba 2018, umetumia takwimu kutoka taasisi za Serikali kwa nchi husika, Shirika la Kazi Duniani (ILO), Benki ya Dunia (WB) na takwimu za UN.

 


Advertisement