Nchi nyingine yaruhusu kilimo, matumizi ya bangi kutibu

Tuesday February 19 2019

Wabunge nchini Cyprus wamepiga kura ya kuhalalisha ulimwaji wa bangi na matumizi kwa ajili ya matibabu, wakiingia kwenye wimbiu kubwa miongoni mwa nchi za Ulaya kuhalalisha mmea huo.

Mabadiliko katika sheria inayosimamia matumizi ya dawa yameingiza vipengele vinavyoruhusu uagizaji wa mbegu na mimea ya bangi kwa ajili ya kilimo kwa sababu za kimatibabu.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, leseni itatolewa kwa wazalishaji watatu kwa miaka 15 ya kwanza kwa lengo la kuvutia makampuni yenye rekodi nzuri kimataifa kudhibiti bangi kuingia kwenye soko lisilo halali.

Bangi kwa ajili ya dawa itaruhusiwa kwa maelekezo ya daktari kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na maumivu sugu, yakiwemo yanayotokana na saratani, Ukimwi, ugonjwa wa mifupa na glaucoma, ugonjwa unaotanua mboni ya jicho.

Wataalamu wamekisia kuwa Cyprus inaweza kujikuta ikizalisha bangi zinazofikia dola 200 milioni za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh450 bilioni za Kitanzania) kila mwaka na hivyo kuisaidia serikali.

Chama cha Green kimefurahia uamuzi huo kikisema: "Tunatumani kuwa mchakato utazinduliwa mara moja kwa ajili ya maelfu ya wagonjwa wanaotafuta njia mbadala, isiyotumia dawa kushughulikia matatizo yao ya kiafya."

"Ingawa tulipendekeza mambo mengi zaidi katika sheria hii, tunaamini kwamba njia ya kuelekea kupata bangi ya dawa imefunguliwa nchini Cyprus," iliongeza.

Zaidi ya nchi 12 za umoja wa Ulaya zimehalalisha matumizi ya bangi kuwa dawa.

Mwezi Novemba, Ugiriki ilitoa leseni ya kwanza ya kulima na kuchakata bangi kwa ajili ya kuzalisha dawa.

 

 


Advertisement