Ndege ya ATC ilivyotekwa kushinikiza Nyerere ajiuzulu (11)

Muktasari:

  • Februari 26, 1982 nchi ilitikisika baada ya kutokea taarifa kuwa ndege ya Shirika la Usafiri wa Anga Tanzania (ATC) imetekwa. Lilikuwa ni tukio la kwanza la aina yake kuwahi kutokea nchi hii na kuzua mijadala kote duniani. Ndege hiyo iliyokuwa ikijiandaa kutoka Uwanja wa Mwanza, ililazimishwa kwenda Nairobi, baadaye Jeddah (Saudi Arabia), Athens (Ugiriki) na safari kuishia Uwanja wa Stansted, Uingereza ambako baada ya mazungumzo na maofisa wa Uingereza, balozi wa Tanzania na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Oscar Kambona, watekaji walijisalimisha. Baadaye watekaji hao, ambao ni vijana watano wa Kitanzania, walishtakiwa katika mahakama ya Uingereza na kuhukumiwa kifungo cha jumla ya miaka 27. Jana tuliona jinsi vyombo vya habari duniani vilivyojadili hukumu na kesi hiyo. Leo tunaangalia yaliyojitokeza wakati wa ushahidi kwenye kesi hiyo.

Pamoja na kwamba awali Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, John Malecela, alisema walioiteka ndege hiyo hawakutoa madai yoyote, kesi iliyomalizika nchini Uingereza iliyowakabili watekaji watano ilifunua mengi yaliyokuwa yamefunikwa.

Kati ya mambo yaliyojitokeza katika kesi hiyo ni utetezi uliotolewa na kiongozi wa watekaji hao, Musa Memba, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 25.

Memba, ambaye alifariki mapema mwaka huu, aliibua jambo ambalo halikuwahi kusemwa kabla baada ya kuiambia mahakama hiyo kuwa utekaji huo ulifanywa kufanikisha mpango wao wa kutoroka nchi baada ya mkakati wa awali wa kushinikiza Mwalimu Julius Nyerere ajiuzulu kugundulika.

Mahakama hiyo iliambiwa kuwa wakati wa maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Tanganyika, Jumatano ya Desemba 9, 1981, watu waliokuwa wakijiita “Harakati za Kidemokrasia Tanzania” walipanga kuteka kituo cha redio ya Serikali cha Redio Tanzania Dar es Salaam.

Alisema kama wangefanikiwa kuteka kituo hicho, wangekitumia kupaza sauti zao kumwambia Rais Nyerere ajiuzulu. Walisema wangefanya hivyo wakati Rais Nyerere akijiandaa kulihutubia Taifa kupitia redio hiyo kutokea Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Memba alisema waliamini kwa kufanya hivyo, sauti yao ingesikika nchi nzima na ndipo kungefanyika “mapinduzi ya kidemokrasia ya watu”.

Hata hivyo, pamoja na hayo, inadaiwa kuwa siku hiyo Mwalimu Nyerere hakufika uwanjani ingawa alisikika redioni akilihutubia Taifa.

Baadhi ya wanachama wa kikundi hicho cha wanaharakati walinaswa na polisi, lakini Memba na wenzake wanne walikimbilia mafichoni hadi walipopata mwanya wa kuingia kwenye ndege hiyo ya ATC aina ya Boeing 737 kwa kutumia uwanja wa Mwanza ambako walijua kuwa hakukuwa na ulinzi wa kutosha.

Memba alidai kuwa katika kuiteka ndege ya ATC, yeye na wenzake hawakuwa na nia ya kumdhuru mtu yeyote ndio maana walikuwa wamebeba bastola ya bandia iliyotengenezwa na wachonga vinyago wa Dar es Salaam. Alisema walichotaka ni kuikimbia Tanzania tu.

Naye wakili wa upande wa utetezi, De Souza, aliyekuwa akimwakilisha Mohamed Tahir Ahmed na Yassin Memba, alisisitiza kuhusu umuhimu wa vijana hao kutoroka nchi alipoieleza mahakama uzuri wa kuwa na uhuru na ubaya wa kutokuwa nao.

“Ulimsikia Bwana Matius Kambona akikwambia kuwa kaka yake, Oscar Kambona, aliukimbia utawala wa Tanzania wakati akiwa bado ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na akiwa angali na heshima na faida nyingi katika serikali yake,” alisema De Souza akinukuliwa na jarida la Africa Now la Aprili, 1982.

“Watano hawa wanaoshutumiwa (kwa utekaji), sasa wako mbele yako hapa kuomba hifadhi ya kisiasa kwa kutumia utekaji nyara.”

Wakili mwingine wa utetezi, Loui Blom Cooper, aliyemwakilisha Musa Memba, Abdallah Ali Abdallah na ndugu yake, alisema mwanzoni washtakiwa waliingia kwenye ndege na bunduki na mabomu ya bandia, kwa hiyo hawakukusudia kuwadhuru abiria wala watumishi wa ndege.

Alisema rubani msaidizi alipigwa risasi na Musa Memba kwa bahati mbaya na alimuomba radhi kwa kuonyesha kusikitishwa kwake na kitendo alichofanya.

Sir Blom-Cooper, ambaye wakati wa kesi hiyo alikuwa na umri wa miaka 56, alifariki dunia Jumatano ya Septemba 19, 2018 akiwa na umri wa miaka 92.

Baraza la wazee 12 waliochaguliwa kumsaidia hakimu kufikia uamuzi wa kesi hiyo (kukiwa na wanaume sita na wanawake sita) hawakuridhishwa na utetezi uliotolewa, badala yake walitumia muda wa saa zisizozidi mbili kutoa hukumu ya kuwatia hatiani washitakiwa wote.

Hukumu hiyo ilikuja miezi saba baada ya ndege hiyo kutekwa ikiwa Mwanza.

Baada ya kutumikia adhabu zao, Alhamisi ya Novemba 14, 1985 ofisi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza ilimwandikia barua Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Jumuiya ya Madola, Geoffrey Howe, ikimkumbusha kuhusu watekaji wa ndege ya Tanzania. Barua hiyo ilimsihi kutafakari kutowarejesha watekaji hao nchini Tanzania bali wapatiwe hifadhi ya kisiasa.

Kesho tutamalizia mkasa huu kwa kuangalia jinsi vyombo vya habari vya Tanzania vilivyoripoti suala hilo