Ndege za Rais Tanzania kuanza kubeba abiria

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Ijumaa ameongoza Watanzania kupokea ndege ya pili aina ya Airbus A220-300 iliyotokea  Canada na kuagiza ndege mbili kati ya tatu za  Rais zianze kupakia abiria.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema ndege mbili za  rais zinapaswa kuanza kutumika kubeba abiria katika siku ambazo hazitakuwa zikitumika.

Amesema ndege hizo zinatakiwa kupakwa rangi kama za ndege za Serikali zilizokodishwa kwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), tayari kwa kuanza safari za kupakia abiria.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Januari 11, 2019 wakati wa mapokezi ya ndege ya pili aina ya Airbus A220-300 iliyowasili katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam.

Amesema badala ya ndege hizo kukaa bila kutumika ni bora zitumiwe kusafirisha abiria kwenda sehemu mbalimbali ili kuhakikisha wigo wa kukuza utalii unaongezeka.

“Kwa kuwa rais mwenyewe hasafiri hovyo sasa zinakaa kufanya nini na moja ina uwezo wa kubeba watu 50. Hii haitabeba abiria pale tu ambako itakuwa inatumika,” amesema Rais Magufuliu.

Akijibu ombi la Askofu mkuu wa kanisa la Full Gospel Bible fellowship (FGBF) Zachary Kakobe aliyemuomba kuwa na desturi ya kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kama ilivyo kwa viongozi wa dini, Magufuli amesema anaogopa kukutana na watu ambao wanatukana na kutishia kumkatakata.

“Huwezi kukutana na mtu anayekuambia akikushika atakukata halafu ukutane naye kumbe ndiyo siku yako ya kuchinjwa hivyo ni bora umuache akae mwenyewe huko,” amesema Rais Magufuli.