Ndugai: Masele aripoti bungeni Jumatatu saa 5, akikaidi atakamatwa

Sunday May 19 2019

 

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele anatakiwa kufika mbele ya Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge kesho Jumatatu kabla ya saa tano asubuhi.

Akizungumza na Mwananchi jana Ndugai alisema ikiwa mbunge huyo hatofika ndani ya muda huo litatolewa agizo la kumkamata na kumfikisha katika kamati hiyo.

Masele ameibua sintofahamu baada ya kutuhumiwa kugonganisha mihimili ya nchi na kwa kile ambacho Ndugai alikiita kufanya mambo ya hovyohovyo, hivyo kuitwa arejee nyumbani na Spika huyo kutoka Afrika Kusini alikokuwa anahudhuria vikao vya Bunge la Afrika (PAP).

“Mwisho Jumatatu, saa tano asubuhi awe ameshafika na ikiwa hajafika itatolewa hati ya kukamatwa kwa sasa bado ni mtu wa kawaida,” alisema Ndugai.

Alipoulizwa kama ana uwezo wa kumtaka Masele kurejea nchini na kuandika barua kwa PAP kusimamisha kwa muda ubunge hadi itakapotolewa taarifa nyingine, Ndugai alisema, “Unapokuwa mwakilishi wetu sisi ndio tumekupeleka, si wale (PAP) ndio wamekuchukua huku.” Aliongeza, “anayesaini barua ya kwenda huko ni nani…, Spika sasa kama ni hivyo kwa nini nishindwe kukurudisha. Yaani rais umteue waziri halafu ushindwe kumtengua. Tulimtaka arudi anapaswa kurudi.”

Ndugai alisema uwezo ambao hana kwa Masele ni kumfukuza ubunge wake wa Shinyanga Mjini. “Alichaguliwa na wabunge ndani ya Bunge lakini kumsimamisha na kumrudisha anatakiwa katika mahakama ya Bunge uwezo huo ninao, lengo ni atoke huko arudi ni lazima tusimamishe unachokifanya ili lengo urudi. Anasahau kuwa anawakilisha nyumbani, wakikuita nyumbani lazima uende,” alisema.

Advertisement

Wakati Ndugai akieleza hayo mbunge wa Momba (Chadema), David Silinde ambaye pia ni mbunge wa PAP alisema: “Nimezungumza na Masele amesema atazungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka katika kamati ya maadili ya Bunge Jumatatu (kesho).”

Akizungumzia suala hilo Dk Richard Mbunda wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema kwanza, kama ni suala la maadili hakukuwa na sababu ya kuvutana katika vyombo vya habari hatua iliyojenga taswira mbaya ya Tanzania katika duru za kimataifa.

“Masele ni makamu wa Rais PAP, vitu vinavyoonekana nje ni kwamba anapigania vitu vinavyomjengea heshima yeye na hata Tanzania katika duru za kimataifa, sasa huo mvutano hauleti picha nzuri, kumbuka hili suala linafuatiliwa na nchi nyingi duniani kwa hiyo wanatushangaa inakuwaje tena viongozi wetu wanaingia kwenye mgogoro,’’ alisema Dk Mbunda.

Mwanaharakati Gemma Akilimali ametilia shaka, akisema huenda Ndugai alitoa tuhuma kwa Masele bila kujiridhisha, akihusisha na sakata la CAG Profesa Mussa Assad aliyeendelea kushikilia msimamo wake kuhusu madai ya ‘udhaifu wa Bunge’

“Ya CAG ilikuwa hivyo hivyo na akafanya wabunge kupoteza mwelekeo lakini sasa si wameaibika? Kwa hiyo inawezekana Ndugai anataka kutumia rungu lake bila kujiridhisha, namshauri anapopata taarifa achukue muda kujiridhisha, kujifunza, afanye consultation (ashauriane) na wengine kabla ya kutumia rungu lake la kiongozi, hakimu hujiridhisha kwa muda kabla ya kutoa hukumu,”alisema.

Alichokisema Masele

Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW) juzi Masele alisema msimamo wa kuunda tume ya uchunguzi dhidi ya Rais wa PAP, Roger Dang aliyetuhumiwa kwa rushwa na matumizi mabaya ya madaraka ndiyo chanzo cha kuingia mgogoro na Ndugai.

Wakati wa uchunguzi huo, tayari Masele alikuwa akikaimu nafasi ya Rais wa Bunge hilo, akisema ripoti imeshakamilika na inaonesha Dang alikuwa na kesi za kujibu.

“Mimi nimeunda tume kumchunguza Rais wa Bunge la Afrika anayetuhumiwa kwa rushwa, matumizi mabaya ya ofisi, undugu, tuhuma za ngono , ripoti (uchunguzi) ilitakiwa iwekwe jana ndani ya Bunge na kujadiliwa.”

“Kwa hiyo huyo Rais (Dang) akijua mimi makamu wa kwanza wa Rais na anatambua misimamo yangu, na sipendi mambo ya hovyo hovyo, akaamua kumtumia Spika wetu wa nyumbani ili aweze kuniita haraka nishindwe kuwepo hapa Afrika Kusini kuongoza vikao ambavyo vingejadili ripoti ya uchunguzi, hiyo ndiyo sababu kubwa,” alisema Masele ambaye pia alikubali kutii agizo la kurejea nchini kuhojiwa na kamati mbili zilizoandaliwa ndani ya Bunge ikiwemo kamati ya maadili ya CCM.Nyongeza na Kelvin Matandiko

Advertisement