Ndugai aitaka Serikali kutoa kauli mauaji ya watoto Njombe

Muktasari:

  • Spika wa Bunge, Job Ndugai ameiagiza Serikali kutoa kauli kuhusu mauaji ya watoto yanayoendelea mkoani Njombe kabla ya kuahirishwa kwa mkutano wa Bunge Ijumaa Februari 8, 2019

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai ameiagiza Serikali kutoa kauli kuhusu mauaji ya watoto yanayoendelea mkoani Njombe kabla ya kuahirishwa kwa mkutano wa Bunge Ijumaa Februari 8, 2019.

Ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu Februari 4, 2019 kufuatia mwongozo ulioombwa bungeni na mbunge wa Lupembe (CCM), Joram Hongole aliyetaka Bunge kuahirisha shughuli zake za leo ili kujadili mauaji hayo.

Mbunge huyo amesema taharuki imezuka mkoani Njombe na shughuli za uchumi zimesimama baada ya mauaji ya watoto chini ya miaka 10 wapatao saba.

“Kumezuka taharuki kubwa na shughuli za uchumi hazifanyiki, wakinamama wanatakiwa kuwapeleka watoto wao shuleni na kuwarudisha jioni,” amesema.

Amesema hali ni mbaya katika mkoa wa Njombe na kwamba kuna watu wanachochea hasira kwa kutuma picha za kuonyesha mauaji mkoani humo.

Mbunge wa Makambako (CCM) Deo Sanga amesema hali ya Njombe ni tete na baadhi ya watu wageni wanaonekana wamekuja kuteka na kuua.

Amesema wafanyabiashara wakubwa 10 wenye watumishi zaidi ya watu 200 wamekamatwa na hivyo shughuli za uchumi zimesimama.

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama amesema jambo hilo ni zito na linachukua taswira nzito ndani ya Taifa.

“Sisi kama Serikali ili tuweze kutoa maelezo ya kina tunaomba utupe nafasi tuandae taarifa na kueleza hatua kubwa ambayo Serikali imechukua ,”amesema

Akijibu mwongozo huo, Spika Job Ndugai amesema ni jambo kubwa linalohuzunisha na kusikitisha na kuagiza kabla Bunge kuahirishwa wanataka kupata maelezo ya juu ya nini kinachoendelea mkoani humo na kisha kuangalia nini cha kufanya.