Ndugai amtaja tena Masele, wabunge watofautiana

Saturday May 18 2019

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa akiomba mwongozo bungeni jijini Dodoma jana kuhusu kusimamishwa kwa uwakilishi wa mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele katika Bunge la Afrika bila ya kujadiliwa na wabunge. Picha na Ericky Boniphace 

By Elias Msuya na Ibrahim Yamola, [email protected]

Dar/Dodoma. Spika Job Ndugai amesema mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele atahojiwa na kamati ya wabunge ya chama chake na si kamati ya maadili ya chama hicho tawala.

“Katika uendeshaji wa mabunge kuna Bunge kama Bunge na mambo yake, pia tuna tambua caucas za vyama tuna uongozi wa vyama vyenye wabunge bungeni na vikao vyao tunaviratibu sisi,” alisema Ndugai jana akijibu swali aliloulizwa na Mwananchi kuhusu kauli yake aliyoitoa juzi bungeni akiamuru mbunge huyo arejee nchini kutoka Afrika Kusini anakohudhuria vikao vya Bunge la Afrika (PAP) baada ya kuzungumza mambo ya aliyosema yanagonganisha Mihimili ya Dola na kwamba atahojiwa na kamati ya maadili ya CCM na ya Bunge.

Wakati Ndugai akieleza hayo, wabunge na wachambuzi walikuwa na maoni tofauti kuhusu uamuzi huo, “ndio maana bungeni huwa tunatangaza Chadema wakutane ukumbi namba fulani. Kwa hiyo kuna mawasiliano kati ya vyama na Spika katika baadhi ya mambo.

“Ninafahamu kutakuwa na kikao cha maadili cha upande wa chama chake cha CCM kwa hoja zao wao nyingine. Inawezekana si kwa hoja za maadili ya Bunge. Ninachoitisha mimi Spika ni cha maadili ya Bunge, kwenye chama ataitwa na wenye mamlaka ya kufanya hivyo ila si CCM Taifa,” alisema Ndugai.

Alifafanua, “caucas ni chombo kinachotambulika hata CCM. Watu hawajui kuwa vyama pia huwa vinajiendesha hata humu ndani (bungeni).”

Alipoulizwa kuhusu kuwa na uhusiano na Rais wa PAP, Roger Nkodo Dang aliyeingia katika mgogoro baada ya tuhuma mbalimbali, alikana.

Advertisement

Huku akieleza kuwa Masele akishahojiwa na kamati hiyo ya Bunge ndipo ukweli utajulikana, Ndugai alisema, “uhusiano na mtu wa Cameroon (Rais wa PAP) umetoka wapi, yeye ni rais na Masele yupo naye huko.”

“Tanzania (Rais wa PAP) alipokelewa mara moja kuomba kura ambako yeye alipata na Masele. Alikuja Dodoma, nilionana naye kwa nusu saa akaondoka. Niliwahi kuhudhuria mkutano Rwanda lakini yeye alikuwa mbele mimi nyuma na hatuna uhusiano wowote.”

Wabunge

Akizungumzia suala hilo, mbunge wa Rufiji (CCM), Mohamed Mchengerwa alisema hakuna tatizo kwa mtu yoyote kupelekwa kamati ya maadili.

“Tatizo hatujui kwa undani hasa tuhuma ambazo Masele anakabiliwa nazo, lakini tuhuma haziwezi kumweka matatani, akifika huko kwenye kamati ataeleza undanina kamati itatoa uamuzi.

Mbunge wa Tandahimba (CUF), Katani Katani alisema, “Masele amechaguliwa (PAP) na wabunge ambao ndio wapigakura wake, kama ana makosa wapigakura wake wanapaswa kujua kwanza si kufichaficha.”

“Kama anagonganisha mihimili, tunapaswa kujua ameigonganishaje hiyo mihimili, kwa hiyo Spika alitakiwa kutueleza hasa makosa yake ni yapi na sio kutuacha njia panda,” alisema Katani.

Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga alisema, “alichokosea Masele ni kuzungumza mbele ya hadhara kuwa Waziri Mkuu amemtaka kubaki huko hii inaonyesha huko nje kwamba sisi hapa hakuna maelewano kati ya Spika na Waziri Mkuu au Serikali na Bunge.”

Mbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe alisema kila Bunge lina taratibu zake, “na kabla ya Spika Ndugai kumtaka kurejea nchini alipaswa kutueleza sisi tuliomchagua.”

Wachambuzi

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Marcossy Albanie alisema hakuna kosa la moja kwa moja la Masele, “hapo kuna siasa zinachochewa tu. Hakuna kosa la moja kwa moja ndiyo maana Spika hajataja.”

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya sera za uchumi na utawala (GEPC), Moses Kulaba alisema kuna upungufu katika utaratibu wa kuwapata wabunge wanaoiwakilisha Tanzania katika mabunge ya kikanda.

“Kwa sababu wanachaguliwa na wabunge wenyewe na baada ya hapo Spika anaandika barua ya kuwatambulisha. Ndipo anapopata nguvu ya kumwita mbunge wakati wowote, maana yuko chini yake,” alisema.

Hata hivyo, alisema mbunge anayekwenda kwenye mabunge ya kikanda, anaiwakilisha nchi hivyo anapaswa kupeleka kile alichoambiwa na nchi anayotoka.

Alisema faida ambayo Tanzania inaipata kwenye mabunge hayo ni pamoja na kujitangaza na kuwa na nguvu ya kupenyeza ajenda itakazotaka.

Advertisement