Ndugai amuita Lissu, asema hana kibali kukaa nje ya nchi

Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai amemtaka mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kurejea nyumbani kwa kuwa hana kibali cha kuwa nje ya nchi.

Ndugai alitoa kauli hiyo jana alipoulizwa na Mwananchi kuhusu waraka uliotolewa na Lissu alioupa jina la ‘Baada ya risasi kushindwa, sasa wanataka kunivua ubunge’.

Lissu, ambaye amemaliza matibabu yake nchini Ubelgiji na sasa anafanya ziara katika nchi za Ulaya amedai kuwa kuna mkakati wa kumvua ubunge akidai Bunge nalo linashiriki katika mpango huo.

Lissu ambaye amepona majeraha aliyopata baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana mwaka juzi, amedai kigezo kinachotaka kutumika kumvua ubunge ni utoro bungeni.

“Ni taarifa gani ya maandishi watu hawa wanahitaji wakati nilishambuliwa nikiwa kwenye vikao vya Bunge Dodoma. Wakati wote ambao nimekuwa kwenye matibabu uongozi wa Bunge umewasiliana kwa maandishi na mwakilishi wa familia yangu kuhusu matibabu yangu. Wametoa matamko mengi hadharani kuhusu kushambuliwa kwangu na kuhusu matibabu yangu” ameandika Lissu katika waraka wake huo.

Lissu alishambuliwa mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake Area D, mjini Dodoma wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge.

Alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na siku hiyo hiyo usiku alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Alipata matibabu katika hospitali hiyo hadi Januari 6, mwaka jana alipohamishiwa Ubelgiji alikohitmisha matibabu yake Desemba 31, mwaka jana. Mwanasheria huyo wa Chadema ametibiwa kwa jumla ya siku 480 sawa na mwaka mmoja na miezi mitatu na siku 24.

Lissu, ambaye siku nne zilizopita alihojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kutoka London, Uingereza na kuzungumza masuala mbalimbali ikiwemo usalama wake, amedai mpango huo wa kumvua ubunge kamwe hautafanikiwa.

Alichokisema Ndugai

Mwananchi lilimtafuta Ndugai na kumuuliza kuhusu kauli ya mbunge huyo na Spika akajibu kuwa, “Huo ni uzushi.”

Ndugai alisema Lissu anapaswa kutambua kuwa hana ruhusa ya kuzurura nje ya nchi.

“Yeye ametoka kuugua aache uzushi arudi nyumbani, tunamsubiri nyumbani. Kitu muhimu ni kwamba ajue hana ruhusa ya Spika ya kuwa huko anakozurura. Sasa achunge kidogo, maana Spika ana nguvu zake, asimpe sababu,” alisema Ndugai.

Ndugai alisema hawezi kumpangia Lissu mambo ya kusema ila ajue hana kibali cha kuendelea kuwa nje ya nchi wakati ofisi ya Spika haina taarifa.

“Wakati wenzake tuko bungeni tunafanya kazi za wananchi yeye yuko huko, sasa hilo kwa taratibu za kibunge ni kosa. Kwa hiyo arudi nyumbani aache maneno maneno nje huko.”

Alipoulizwa muda sahihi wa Lissu kuendelea kupata matibabu nje ya nchi, Spika Ndugai alisema atakuja kutoa taarifa maalumu juu ya suala hilo. “Wewe usinitangulie bwana nitatoa maelezo kuhusu inavyokuja, eeh kama anakuwa penalized (adhibiwa) nitasema,” alisema Ndugai.

“Lakini muhimu awahi kurudi nyumbani. Akishaingia kuvunja kanuni zangu atajikuta yuko nje ya uwanja, sasa asifike huko. Muhimu kurudi nyumbani na kufanya kazi ambayo wananchi wametupa, badala ya kuzunguka nje na kuipaka matope nchi.”

Madai ya Lissu

Katika waraka huo Lissu alisema, hawezi kupuuza taarifa alizoambiwa na watu wake wa karibu kuhusu kuvuliwa ubunge.

“Nimepata taarifa kutoka kwa watu wawili tofauti kwamba kuna mkakati unaandaliwa wa kunivua ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki,” ameandika Lissu.

“Yaani sijamwandikia katibu wa Bunge taarifa yoyote ya maandishi kuhusu kuumwa kwangu wala matibabu yangu, kwa maneno mengine, sijahudhuria vikao vya Bunge tangu tarehe 7 Septemba 2017 hadi sasa bila sababu au taarifa yoyote rasmi,” alisema Lissu.

Lissu alisema hashangazwi na taarifa hizo, akidai kuwa ni mwendelezo wa chuki na visasi.

“Nilipelekwa Nairobi nikiwa sijitambui kutokea Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma, baada ya kikao kilichomshirikisha katibu wa Bunge wakati huo Dk Thomas Kashilillah, Spika Ndugai na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.”

Lissu alieleza jinsi viongozi mbalimbali waliomtembelea alipokuwa Nairobi, akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan huku akinukuu taarifa za Bunge kuwa ingepeleka timu ya madaktari kumjulia hali, hivyo anashangaa kusikia hayupo bungeni kwa sababu ya utoro.

“Na waandikiwe barua gani zaidi ya barua nne au tano ambazo wamekwishaandikiwa na kaka yangu wakili Alute Mughwai na ambazo wameshazijibu,” alihoji.