Ndugai amvaa Zitto uchambuzi taarifa za CAG

Thursday April 25 2019

 

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Wakati Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe akitumia majukwaa mbalimbali kuchambua ripoti ya ukaguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kwa mwaka wa fedha 2017/18 ulioishia Juni mwaka jana, Spika wa Bunge, Job Ndugai amemtaka kuacha kuwaaminisha Watanzania kuwa kila kilichomo katika taarifa hizo kina ukweli.

Ndugai ametoa kauli hiyo leo mchana Alhamisi Aprili 25 bungeni jijini Dodoma muda mfupi kabla ya kuahirishwa kikao cha Bunge hadi jioni.

“Zitto hayupo hapa amekuwa mwepesi akitoa taarifa hasa katika vitabu vya ofisi ya ukaguzi wa taifa na watu wengi wanamtafsiri kama shujaa kwa sababu waliopo nje ya Bunge hawaelewi taratibu zetu.”

“Kwa kawaida taarifa za ukaguzi za CAG kwa utaratibu wetu zikiwekwa mezani zitakwenda kamati ya Bunge ya PAC (Hesabu za Serikali) na LAAC (Hesabu za Serikali za Mitaa). Kwenye kamati kule watachambua kila kitu hoja kwa hoja,” amesema.

Amesema katika kamati hiyo wote waliotajwa katika taarifa hizo wataitwa kwa ajili ya kutoa maelezo mbalimbali, huku akitolea mfano sakata la sare za polisi na hata ununuzi wa gari la Chadema uliotajwa katika ripoti za CAG.

“Kama nilivyosema wakati fulani zile ni hoja, lakini watu wanawaaminisha Watanzania kuwa kila kichoandikwa na CAG mle ni ukweli asilimia mia moja. Yapo mambo mle si kweli hata kidogo tena mengi tu.”

Advertisement

“Mengine utakuta kiambatanisho tu hakipo na mifano ipo mingi, yaani kitabu huchambuliwa na wakati mwingine zinabaki hoja chache ndio tunawapa Serikali au polisi kama zinahusu huko. Anachokitaka Zitto ni kuendelea kuwa mwenyekiti wa PAC kinyemelela.”

 “Unawaaminisha wananchi nchi nzima kuwa kuna mahela sijui wapi. Mfano Halmashauri yake (ya Kigoma Ujiji-inayoongozwa na ACT-Wazalendo) imetajwa kuwa na hatI chafu nayo itaitwa. Lazima kila aliyetajwa katika ripoti ajibu,” amefafanua.

Ndugai amesema Zitto amekuwa akizichukua taarifa hizo kama zilivyo ili aonekane kuwa anaweza kuchambua mambo kuliko wengine.

“Hatumkatazi kwa sababu havunji kanuni yoyote, ila ni vizuri tukajua taratibu. Katika maisha tusipende sana kutuhumu watu, wape nafasi waliotajwa wajieleze na kama hawana maelezo sasa toka nje huko ndio useme,” amesema Ndugai.

Amesema ukifikia wakati wa kuitwa watu waliotajwa katika ripoti hiyo wote watatakiwa kutekeleza agizo hilo na wakigoma watapelekwa hata kwa pingu.

Advertisement