Ndugai apigia chapuo Bunge rasmi la SADC

Tuesday August 6 2019

Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza wakati

Spika wa Bunge, Job Ndugai akizungumza wakati wa hafla ya chakula cha jioni juzi usiku kilichoandaliwa kwa ajili ya wajumbe wa wiki ya maonyesho ya Sadc. Picha na Anthony Siame 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amewaomba viongozi kuoka Nchi 16 za Jumuiya ya Maendelo ya Kusini mwa Afrika(SADC), kuunga mkono pendekezo kufanya jukwaa la wabunge kuwa Bunge rasmi la SADC litakalokuwa na uwezo wa kutunga sheria.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo jana usiku Jumatatu Agosti 5,2019 wakati wa chakula cha jioni kwa washiriki wa maonyesho hayo ya viwanda kwa nchi 16 za SADC, kilichoandaliwa na wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

“Bunge la Tanzania limekuwa mstari wa mbele katika kuimarisha mtangamano wa SADC kupitia jukwaa la Bunge la SADC ambalo wabunge wetu (Tanzania) wanashiriki.”

“Jukwaa hilo limekuwa likitumika kujadili masuala yanayohusu maslahi ya nchi wanachama wa SADC, ikiwamo utekelezaji wa itifaki ya bidhaa, madini, sayansi na teknolojia, kilimo, utalii, na kadhalika,” alisema Ndugai.

Kiongozi huyo wa Bunge alisema, “Kwa kuona umuhimu wa jukwaa hilo, (SADC Parliamentary forum), Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kutetea jukwaa hili ili siku zijazo liweze kuwa Bunge kamili la kikanda. Ningependa kutoa wito kwa nchi nyingine wanachama kuunga mkono hoja hii ya kuanzisha kwa bunge hili litakalokuwa chombo madhubuti kuimarisha mtangamano huu.”

Aidha, Ndugai alipongeza juhudi za Rais wa Tanza, John Magufuli ambaye Juni 28, 2019 alipokea ujumbe maalumu wa maspika wa Bunge la Nchi za SADC uliowasilishwa na Spika wa Bunge la Msumbiji na Rais wa Jukwaa hilo la SADC, unaopendekeza kuwa bunge kamili la SADC.

Advertisement

“Ni matumaini yetu kwa mkutano unaokuja wa wakuu wa nchi 16 za SADC pamoja na mambo mengine utazingatia maoni haya kutoka kwa wabunge hao wa jukwaa la SADC,” alisema Ndugai ikiwa siku ya kwanza ya maonyesho ya bidhaa katika wiki ya viwanda itakayofikia ukomo wake Ijumaa wiki hii.

Maonyesho hayo kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2016 nchini Eswatini, mwaka 2017 nchini Afrika Kusini , mwaka 2017 nchini Namibia na awamu ya nne mwaka huu nchini Tanzania ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa awamu ya kwanza 2015/30 ya Mkakati wa Viwanda wa SADC 2015/2063.

Kwa mujibu wa SADC, Mkakati huo umejikita katika maeneo makuu matatu ambayo ni viwanda, ushindaji na Mtangamano wa Kikanda.

Advertisement