Ndugai atoa agizo kwa Waziri Mkuu kuhusu Watanzania kupewa saa 24 kuondoka Kenya

Muktasari:

  • Charles Njagua Kanyi maarufu Jaguar ni mbunge wa Starehe na mwanamuziki maarufu ndani na nje ya Kenya. Video iliyosambaa mitandaoni kuanzia jana Jumatatu Juni 24, 2019 inamuonyesha akitoa saa 24 kwa raia wa kigeni waliopo nchini humo, wakiwemo Watanzania kurejea makwao na ikiwa hawatafanya hivyo, wananchi wa Kenya watavamia maeneo yao, yakiwemo ya biashara.

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amemtaka Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo jioni Jumanne Juni 25, 2019 kutoa majibu ya Serikali kuhusu kauli iliyotolewa na mbunge wa Starehe nchini Kenya, Charles Njagua Kanyi maarufu Jaguar aliyewapa saa 24 Watanzania waishio nchini humo kurejea makwao.

Video inayosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii inamuonyesha Jaguar ambaye pia ni mwanamuziki maarufu ndani na nje ya Kenya, akitoa maagizo hayo huku akiwa amezungumzwa na umati wa wananchi waliomshangilia na kumsindikiza kila eneo alilopita.

Ndugai ametoa kauli hiyo leo Jumanne mchana wakati akijibu mwongozo wa mbunge wa Rufiji (CCM), Mohammed Mchengerwa aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu mbunge huyo.

“Kwa mujibu wa kanuni ya 68 (7) lakini kwa maelekezo yako na ridhaa kwa kanuni ya tano kwa kuwa jambo hili halijatokea bungeni leo ila ni dharura, na kwa kuzingatia jinsi jumuiya za kimataifa zinavyodumisha uhusiano hasa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inavyoendelea kupiga hatua za mahusiano kuimarisha umoja na hata kuondoa mipaka iliyopo,”

“Jana mbunge wa starehe, Charles Njagua Kanyi alitoa  ushawishi kwa Wakenya kuwafukuza wageni wakiwemo Watanzania akitoa saa 24, Serikali inachukua hatua gani  kutokana na matamko haya mabaya kabisa kutokea,” amesema Mchengerwa.

Katika majibu yake Ndugai amesema, “Kwa kuwa nalisikia mara ya kwanza kutoka kwako tuipe muda Serikali ilichukue na tutapata maelezo leo maana huyu mtu ametoa saa 24. Tutakuwa tumejipanga kupata maelezo ya serikali kuhusu usalama wa Watanzania leo jioni,” amesema Ndugai.