Ndugai atoa msimamo hoja ya Zitto sakata la CAG

Thursday January 10 2019

 

By Cledo Michael, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Unaweza kusema Spika wa Bunge, Job Ndugai ameamua kula sahani moja kimataifa na kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Hiyo ni kutokana na leo Alhamisi Januari 10, 2019,  Ndugai naye kuandika waraka kwenda kwa katibu mkuu wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) kutoa ufafanuzi kuhusu barua iliyoandikwa na Zitto jana kwenda katika jumuiya hiyo.

Katika barua hiyo, ambayo Zitto amewatumia pia maspika wote wa nchi wanachama wa CPA na wanasheria wakuu, amesema sakata hilo lilianza baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kusema anaamini kuwa kutotekelezwa kwa ripoti anazozitoa, ni udhaifu wa Bunge.

Wakati barua ya Zitto kwenda kwa katibu mkuu wa CPA, Akbar Khan ikieleza mzozo ulioibuka kati ya Ndugai na Profesa Assad, waraka wa Ndugai umesema Bunge hilo haliwezi kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania.

Zitto, ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini, amesema maoni hayo yamemfanya Spika Ndugai kumtaka Profesa Assad kufika mbele ya kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ahojiwe na kujieleza.

“Mimi binafsi nimeguswa na suala hili. Naomba mabunge ya Jumuiya ya Madola muingilie kati si tu kwa sababu agizo la Spika Ndugai linavunja Katiba bali pia ni hatari kwa mustakabali wa Jumuiya ya Madola kwa ujumla,” ameandika Zitto katika barua hiyo.

Zitto amesema kama CAG ataadhibiwa na kamati ya Bunge kwa kutoa maoni yake, basi ni wazi kwamba uhuru wa Taasisi ya Juu ya Ukaguzi (SAI) utakuwa umevunjwa, kinyume na makubaliano yaliyofikiwa na kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola mwaka 2013.

Ila leo, Ndugai amesema barua ya Zitto imelenga

kuibua taharuki na kwamba uamuzi wake wa kumuita CAG mbele ya kamati ya Maadili si kosa bali ni halali  kisheria.

Katika waraka huo wenye maneno 500, Spika ameeleza kuwa uamuzi alioufanya si kosa na kwamba ana historia kubwa ya kuongoza Bunge katika ngazi za itaifa na kimataifa ikiwamo CPA.

Ndugai ambaye pia mwenyekiti wa maspika na viongozi wa Bunge katika nchi za Jumuiya ya Madola amesema pamoja na kuwa suala la kumuita CAG linaonekana kuwa geni bado ni halali.

Soma Zaidi: Ndugai: Tumempa CAG barua ya wito

“Ni dhahiri kuwa katika mabunge mengine ya Jumuiya ya madola haijawahi kutokea Spika akamuita CAG kwenye kamati ya madili lakini ni wazi kuwa hakuna CAG ambaye aliwahi kuliita Bunge kuwa ni dhaifu,”  amesema Ndugai katika waraka huo.

“Taarifa ya Zitto imepindishwa, mzozo huu umetokea kwa sababu Ndugai amemuita CAG kwenye kamati ya maadili lakini hilo ni jambo la upande wa pili, imetokea kwa sababu CAG ameliita Bunge kuwa ni chombo dhaifu kwenye mahojiano yake na UN Redio nchini Marekani.”

Soma Zaidi: Zitto alifikisha sakata la Spika Ndugai, CAG ngazi za kimataifa

 


Advertisement