VIDEO: Ndugai awapa ahueni wapinzani bungeni kwa masharti

Muktasari:

  • Wapinzani wamefunguliwa milango ya kusoma hotuba zao ndani ya bunge bila ya kuhaririwa, lakini wametahadharishwa kuwa makini kukwepa maneno yenye kusababisha matatizo kwa mihimili na taasisi nyingine

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema kuanzia sasa ni ruksa kwa wapinzani kusoma hotuba zao kama walivyoziandika ingawa ametahadharisha kutokuweka maneno yanayoweza kusababisha migongano na mihimili mingine.

Ndugai amesema hayo leo Alhamisi Aprili 25 wakati akitoa ufafanuzi kuhusu hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani katika wizara ya mambo ya ndani ya nchi, Godbles Lema ambayo ilisusiwa kusomwa jana na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa

Kauli ya Spika imekuja wakati katika mkutano huu wa 15 wapinzani wakishindwa kusoma hotuba mbili ikiwemo ya wizara ya habari ambayo msemaji wake Joseph Mbilinyi aondoe maneno kadhaa.

Jana Msigwa alisema nafsi yake na  wapinzani wenzake inamsuta kama angesoma maoni hayo aliyosema yamehaririwa kwa kiasi kikubwa na akaomba hotuba hiyo apelekewe waziri ili aisome.

“Kabla ya kuendelea naomba nizungumzie jambo moja ambalo lilijitokeza jana na siku za nyuma, hizo hotuba za wenzetu wa upinzani kuna shida kidogo katika uandishi na wakati mwingine zinaleta matatizo makubwa, shida kuna watu wanaandika nje ya bunge na mawaziri vivuli hawazisomi wao wanafika na kusaini tu,” alisema Ndugai.

Amewataka wapinzani hasa wanaosoma hotuba hizo kuwa makini na kuzisoma kabla ya kusaini ili wakibanwa makosa yawe ni juu ya wasomaji wenyewe.

Kiongozi huyo wa Bunge ameagiza hotuba hizo zipelekwe bungeni kama zilivyo kawaida lakini akasema wataendelea kubishana hapo hapo bungeni.