Ndugu wanne wa familia moja akiwemo bibi harusi wafariki ajalini

Wednesday June 19 2019

 

By Godfrey Kahango, Mwananchi [email protected]

Mbeya. Watu wanne wa familia moja wamefariki dunia akiwamo bibi harusi  mtarajiwa na wengine wawili kujeruhiwa kwa ajali ya gari.

Ajali hiyo imetokea alfajiri ya leo Jumatano Juni 19, 2019 eneo la Machimbo barabara kuu ya Mbeya- Zambia ambapo gari lililowabeba wanafamilia hao kupinduka wakati dereva akijaribu kulikwepa lori lililokuwa mbele yao.

Wanafamilia hao walikuwa wakitoka nyumbani kwao Chimala wilayani Mbarali, Mbeya kwenda Jijini Dar es Salam  kwa ajili ya maandalizi ya harusi ya binti yao.

Akizungumza kwa simu, kaka mkubwa wa familia hiyo, Stephano Mwanduga  amesema waliofariki ni wadogo zake ambao ni bibi harusi Diana (28), Faraja Mwandunga, James Mwandunga na mtoto wa Jacton (2) ambaye ni mtoto wa Faraja.

Amewataka waliojeruhiwa ni Ibrana Mwandunga na Nico Mwandunga.

“Wameondoka leo alfajiri kuja Dar es Salaam na walipofika Machimbo ndio wakakutana na gari kubwa hiyo walitaka kulikwepa, basi gari ikawashinda na kupinduka mtaroni,” amesema

Advertisement

“Jumamosi iliyopita ya June 16, 2019 tulikuwa na sherehe (Send Off) ya kumuaga mdogo wetu Diana na Jumamosi ijayo (Juni29) ilikuwa harusi yake. Mimi na ndugu wengi tulitangulia kuja Dar ila yeye na watu wengine walibaki ambao walikuwa katika safari hiyo.”

Amesema bwana harusi Elisante  Edward baada ya Send Off aliondoka kwenda kwa ndugu zake Mbeya Mjini na leo alfajiri alipanda basi la kawaida kwenda Dar es Salaam, lakini baada ya kupata taarifa hizo membedi ateremke Chimala.

Amesema wadogo zake wawili waliojeruhiwa wamepelekwa Hospitali ya Chimala lakini miili ya marehemu wote imepelekwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.

Jitihada za kumpata kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kuzungumzia ajali hiyo zinaendelea.

Advertisement