Ndugu wazuiwa kesi ya kina Maimu, waangua kilio

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Dickson Mwaimu akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza wakati akirudishwa chumba cha mahabusu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana. Mwaimu na wenzake watano wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi. Picha na Omar Fungo

Dar es Salaam. Vilio vimetawala katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya ndugu, jamaa na marafiki wa mkurugenzi mkuu wa zamani wa Nida, Dickson Maimu na wenzake wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kuzuiwa kuingia kusikiliza kesi ya ndugu zao.

Katika kesi hiyo Maimu na wenzake, Avelin Momburi, Astery Ndege, George Ntalima na Sabina Raymond wanakabiliwa na mashtaka 100 likiwamo la utakatishaji fedha haramu Sh1.17 bilioni.

Jana kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya mashaidi, lakini haikufanyika hivyo kutokana na taratibu kutokamilika.

Kesi hiyo ilisomwa katika chumba namba nne cha Hakimu Mkazi Mkuu, Salum Ally lakini ndugu wa washtakiwa hao walizuiwa na askari kuingia kusikiliza kutokana na ufinyu wa chumba hicho na kuzua kizazaa huku wengine wakilia na kulalamika.

Mmoja wa ndugu wa washtakiwa hao, Jamila Ibrahim alisema: “Leo kwa nini kesi hii isomwe kwenye chumba cha mahakama ya ndani badala ya wazi, tulitaka na sisi tusikie nini kinaendelea kwa ndugu zetu.”

Ndani ya Mahakama maofisa wa Takukuru waliiomba Mahakama kumuhoji mshtakiwa wa tano, Xavery Kayombo anayekabiliwa na mashtaka 100 yakiwamo 24 ya utakatishaji wa fedha haramu Sh 1.17 bilioni, ombi ambalo lilikubaliwa.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Februari 19 kwa ajili ya maelezo ya mashahidi.

Kati ya mashtaka 100, mashtaka 24 ni ya kutakatisha fedha, 23 ya kughushi, 43 kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri na matano ya kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh1.175 bilioni.