Ndugulile: Asilimia 67 ya ardhi Kigamboni imepimwa

Muktasari:

  • Mbunge Ndugulile amesema asilimia 67 ya ardhi ya Kigamboni imepimwa, huku mikakati ikiwa kupafanya kuwa kitovu cha biashara

Dar es Salaam. Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk Faustine, Ndugulile, amesema anajivunia kuongoza eneo ambalo ardhi yake asilimia 67 imepimwa.

Naibu waziri huyo wa afya ametoa kauli hiyo leo Jumapili Machi 24, 2019  alipokuwa akigawa mkataba wa ununuzi wa viwanja kwa wananchi wa Mtaa wa Mwasonga, Kata ya Kisarawe2, vinavyouzwa kwa mkopo na kampuni ya KC inayojishughulisha na upimaji na kuendeleza ardhi.

Ndugulile, amesema kitendo cha KC kupeleka mradi huo ni katika kuendeleza juhudi hizo za Serikali na kuahidi hadi kufika mwaka 2020 wana imani ardhi yote itakuwa imepimwa.

"Eneo la kisarawe2 ni la kimkakati kwa ajili ya biashara na tayari eka 1,000 zimetengwa kwa ajili ya viwanda, hivyo mlioamua kununua viwanja hapa hamtajuta kwani huko mbele ya Kigamboni inatarajiwa kuwa kitovu cha biashara katika mkoa wa Dar es Salaam na uwezo huo na sababu tunayo,"amesema Ndugulile.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya KC, Khalid Mwinyi, amesema viwanja hivyo huuzwa kwa mkopo ambapo mteja akishalipa asilimia 20 ya bei ya kiwanja husika, inayobaki analipa kwa miaka miwili.

Mwinyi amebainisha kuwa wamekuja na mkakati huo kama njia ya kuwawezesha wananchi wenye kipato cha chini kumiliki ardhi ambapo leo eka 200 zilizopimwa zimechukuliwa na wananchi zaidi ya 900.

"Moja ya changamoto tuliyoipata katika kupata wateja ni pamoja na suala la wananchi kuamini kama kweli watapata viwanja kwa kile walichodai wameshatapeliwa sana huko nyuma, hivyo tunajitahidi kuwaonyesha sisi hatupo hivyo kwa kuweka kila kitu wazi," amesema.

Naye Naibu Meya wa Ilala, Omar Kumbilamoto, ambaye alimwakilisha mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesema kuna alichojifunza kuhusu umuhimu wa kuwa na maeneo ya kupimwa kutoka Kigamboni, ustaarabu ambao amesema atapeleka elimu hiyo Ilala.

Wananchi waliokabidhiwa mikataba akiwemo Eleotheria Namikowi ambaye ni mkazi wa Mwananyamala na Bashiru Mkabala wa Ubungo, wamesema moja ya jambo lililowashawishi kuchukua viwanja hivyo ni pamoja na kukopeshwa vifaa vya ujenzi.