UCHOKOZI WA EDO : Neno dhaifu linauma kuliko mabilioni yaliyopotea?

Tuesday April 16 2019

 

By Edo Kumwembe

Kama tungekuwa China, wiki hii yule jamaa yao anayenyonga watu wanaoiba fedha za umma angekuwa na kazi nzito. Kuna mabilioni ya fedha yamepotea. Namba Moja alituhimiza tulipe kodi lakini kuna watu bado wana ujasiri wa kula kodi zake.

Namba Moja ameanzisha miradi ya treni ya umeme, amenunua ndege, anajenga barabara nyingi. Haya mambo yanataka fedha nyingi, lakini watu bado wanaiba kiujanja. Baada ya ripoti ya CAG tulipaswa kuwa bize na hesabu ya noti zilizopotea pamoja na watu waliohusika.

Tungekuwa China kuna watu wengi katika mafaili ya CAG ilibidi wanyongwe. Ajabu iliyoje kwamba pambano linalovutia zaidi kwa sasa ni kati ya mkuu wa mjengo wa Dodoma dhidi ya CAG. Juzi mkuu wa mjengo wa Dodoma aliita waandishi wa habari kusisitiza anavyokerwa na neno dhaifu.

Pambano linavutia kwelikweli. Neno ‘dhaifu’ ni habari ya mjini. Pambano hili linachekesha sana. linanikumbusha udhaifu wetu. Jinsi ambavyo tunavyoweza kuweka kando jambo la msingi tukajadili jambo ambalo halina maana sana.

Hoja ya msingi ilipaswa kuwa namna ambavyo mabilioni yanaendelea kupotea. Wajanja bado wanapiga fedha. Watu ambao wanatuhumiwa kwa namna moja au nyingine watakuwa wanavutika na mpambano huu, wanautumia kama kivuli kujificha.

Vichwa vya habari vya magazeti vilipaswa kuandika habari kama vile ‘uchunguzi wa mabilioni yaliyopotea waanza’. Hata hivyo haiko hivyo. Kwa sasa vichwa vya habari vinasema ‘Spika amvaa CAG’. Kichwa kingine cha habari kinasema ‘CAG ajibu mapigo ya Spika’.

Ndani ya habari haukuti neno ‘mabilioni’. Unakuta neno ‘dhaifu’. Tulioishia darasa la saba tunashindwa kuelewa nani anapaswa kushughulikia kinachoendelea baada ya ripoti kuonyesha upotevu wa mabilioni?

Nchi ambayo watu wake wapo makini wangesahau haraka habari ya neno dhaifu na kutupia macho upotevu wa mabilioni, lakini sisi inaonekana bado tunapenda siasa na siku hizi wanasiasa wanajaribu kuwageuza waandishi kuwa shimo la takataka. Kitu kidogo tu utasikia waandishi wa habari wameitwa katika mkutano wa waandishi wa habari. Ukichunguza sana hauoni tija katika mkutano mzima zaidi ya mipasho.

Advertisement