UCHOKOZI WA EDO:Nimerudi tena na kelele za ujenzi wa nyumba

Wananchi wenye hasira walikuja juu majuzi baada ya kupiga soga hapa jinsi ambavyo suala la ujenzi wa nyumba linachukuliwa kama ushujaa kwa wanaojenga. Inaonekana kama ni tafsiri ya haraka ya mafanikio ya maisha ya mwanadamu anayeishi Tanzania.

Kuna watu ambao hawakunielewa vema. Tuna vichwa tofauti. Tatizo hapa nilikuwa nalaumu sera zetu tangu wakati wa Mwalimu Nyerere mpaka sasa. Tulikosea, tukaendelea kukosea na bado tunakosea.

Ni kweli watu wanalazimika kujenga nyumba kwa ajili ya kujihami. Hawana namna. Hawakuandaliwa makazi na serikali au kampuni binafsi ambazo zamani hazikuwepo. Hili ndilo tatizo langu la kwanza la msingi. Kwa nini mwananchi wa kawaida ajenge?.

Matokeo yake tumetumia ardhi vibaya, hatujengi kwa utaratibu. Mfumo wa sasa ni wa mwananchi wa kawaida kumiliki nyumba kwa kununua au kukopa. Hizi kelele za kwenda ‘Site’ kila wikiendi sio suala la kujivunia sana ingawa tunalazimika. Mimi mwenyewe nimejenga.

Kwa ambao wanapata bahati ya kusafiri mara kwa mara katika nchi za wenzetu walioendelea nadhani inabidi tupige kelele za namna ambavyo tunapaswa kufanya kile ambacho wenzetu wamefanya. Hasa katika miji ambayo haijaharibiwa sana kama Dar es Salaam.

Kwa mfano Dodoma ni wakati muhimu sana huu kwa kampuni na mashirika, kujenga ‘apartments’ ambazo zitakodishwa na kisha kuuziwa mabosi wetu wanaohamia kule. Tukisema kila bosi ajenge nyumba yake ina maana Dodoma haitakwenda kwa mipango miji kama ilivyokosewa Dar es Salaam.

Lakini zaidi nikaongea hoja ya pili. Hii nayo ieleweke vema. Kwa nini tunapima mafanikio ya mtu kwa nyumba aliyoacha au alizoacha? Kuna watu wanamdharau Mwalimu Nyerere kwa sababu alijenga nyumba moja tu dhaifu. Yaani licha ya mazuri yote aliyofanya lakini kuna wengine wanapima mafanikio yake kwa nyumba tu aliyoacha.

Nadhani tuna athari za kisaikolojia ambazo zinatulazimisha kuamini kwamba ujenzi wa nyumba ni mafanikio. Hapana sio kweli. Labda iwe sehemu ya mafanikio tu.

Watu wenye asili ya Asia nchini wananufaika kuishi katika nyumba za Msajili wa Maumba pale katikati ya jiji huku fedha zao wakizizungushia katika mitaji lukuki na kupata fedha zaidi.