Nusu ya wanafunzi darasa la saba hawawezi Kiingereza cha darasa la pili

Wednesday December 18 2013

Wanafunzi wakisoma ripoti ya utafiti wa uwezo

Wanafunzi wakisoma ripoti ya utafiti wa uwezo wa wanafunzi kati ya miaka 7-16 wa kusoma na kufanya hesabu, iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam jana na Taasisi ya Twaweza. Picha na Silvan Kiwale 

Dar es Salaam. Asilimia 24 ya wanafunzi wa darasa la saba nchini hawawezi kusoma hadithi rahisi iliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la pili ambapo asilimia 50 ya wanafunzi hao, hawawezi kusoma hadithi ya Kiingereza ya darasa la pili.

Hayo yamebainishwa na ripoti iliyotolewa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Uwezo Tanzania (Twaweza), iliyofanya utafiti nchi nzima kupima uwezo wa wanafunzi wa shule za msingi wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).

Utafiti huo uliozinduliwa Dar es Salaam jana, unaonyesha pia kuwa asilimia kumi na moja ya wanafunzi wa darasa la saba hawawezi kufanya hesabu rahisi za darasa la pili.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Mratibu wa Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla alisema hali ni mbaya zaidi kwa wanafunzi wanaotoka katika familia maskini kulinganisha na wale wanaotoka kwenye familia zenye uwezo.

Aidha, alisema watoto wanaotoka kwenye shule za mjini wanaonekana kufanya vizuri zaidi ikilinganishwa na wale wanaotoka kwenye shule za vijijini.

Alisema utafiti huo ulifanywa kwenye wilaya 126 na kushirikisha kaya 55,191, wanafunzi 104,568 na shule 3,624.

“Kila watoto watano kati ya 10 wa darasa la saba, walishindwa kusoma hadithi ya ngazi ya darasa la pili. Hii ina maana kuwa nusu ya wanafunzi wa darasa la saba hawana misingi ya somo la Kiingereza,” inasema sehemu ya utafiti huo.

Kwa upande wa darasa la tatu, utafiti huo unaonyesha kuwa, ni mtoto mmoja tu kati ya wanne, sawa na asilimia 26 waliweza kusoma hadithi ya darasa la pili ya somo la Kiswahili. Kwa somo la Kiingereza, ni mtoto mmoja tu kati ya 10, sawa na asilimia 13 aliyeweza kusoma hadithi ya Kiingereza ya darasa la pili.

Kwa upande wa hesabu, utafiti huo unaonyesha kuwa ni watoto wanne tu kati ya 10 wa darasa la tatu ambao ni sawa na asilimia 44, waliweza kufanya hesabu ya darasa la pili.

Mkuu wa Taasisi ya Twaweza, Rakesh Rajani alisema wameamua kutumia kigezo cha majaribio ya darasa la pili kwa sababu, sera ya elimu inaelekeza kuwa mtoto akivuka darasa la pili awe na misingi ya KKK.

Sehemu ya muhtasari wa ripoti ya utafiti huo, inasema ingawa kila mtoto nchini anayesoma darasa la tatu au zaidi anapaswa kuwa na uwezo wa kusoma na kuandika vitu vya darasa la pili.Ukweli ni kuwa lengo hili halifikiwi.

“Katika miaka mitatu iliyopita, uwezo wa kusoma na kuandika umebaki chini na kwa kiasi kikubwa na haujabadilika ingawa uwezo wao wa hesabu umeonyesha kuboreka kidogo.”

Advertisement