Nusu ya wabunge hawatarudi bungeni mwakani

Thursday November 13 2014

Bunge likiendelea mjini Dodoma. Picha na

Bunge likiendelea mjini Dodoma. Picha na Maktaba 

By Ibrahim Yamola, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likiendelea na vikao vyake mjini Dodoma, imeelezwa kwamba nusu ya wabunge 239 wa kuchaguliwa waliopo sasa, watabwagwa katika Uchaguzi Mkuu 2015.

Hiyo inatokana na wabunge kutoa ahadi nyingi kwa wapigakura ambazo hawazitekelezi hivyo kukumbwa na rungu la wananchi mwakani.

Hayo ni matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza ambayo yalitangazwa Dar es Salaam jana ambayo yanaonyesha Watanzania wanane kati ya 10 wanawafahamu kwa majina na vyama wabunge hao.

Akiwasilisha taarifa hiyo, mtafiti Elvis Mushi alisema: “Walipoulizwa kama watampigia tena kura mbunge wao wa sasa, karibu nusu ya Watanzania (asilimia 47) walisema hapana, asilimia 47 walisema ndiyo na asilimia tano walisema hawajui.

“Waliosema wasingempigia kura mbunge wao ni wale walioripoti pia kuwa mbunge wao ama ametekeleza ahadi chache au hajatekeleza ahadi yoyote aliyoitoa katika uchaguzi uliopita,” alisema Mushi.

Aliongeza: “Wapigakura wanane kati ya 10 sawa na asilimia 79 wanakumbuka ahadi zilizotolewa na wabunge wao wakati wa kampeni.”

Advertisement

Mushi alisema ahadi nyingi zilikuwa zinahusu ujenzi; kujenga au kukarabati barabara (asilimia 77), kujenga au kuboresha vyanzo vya maji (asilimia 64), ujenzi wa hospitali asilimia 38 na ujenzi wa madarasa katika majimbo yao asilimia 23.

“Kwa bahati mbaya ni mwananchi mmoja tu kati ya wanane, sawa na asilimia 12, aliyeripoti kuwa mbunge wake ametekeleza ahadi zake zote.”

“Asilimia 54 ya wananchi walisema mbunge wao alikuwa ametekeleza baadhi tu ya ahadi zake huku wananchi wanne kati ya 10 sawa na asilimia 38 wakiwa wamefuatilia wenyewe au jamaa zao ndani ya jamii utekelezaji wa ahadi hizo za mbunge wao,” alisema Mushi.

Kuhusu elimu ya mbunge, Mushi alisema watu watatu kati ya wanne sawa na asilimia 74 walisema wangeangalia kiwango cha elimu ya mgombea.

“Nusu ya waliohojiwa wanatarajia mbunge awe na angalau elimu ya shahada, umri wa mgombea na uaminifu wa mgombea, mnyoofu, mkweli au mwadilifu. Kati ya wale waliotaja umri walifikiria mbunge anapaswa kuwa na umri wa miaka 40 au zaidi ambao ni asilimia 55,” alisema Mushi.

Advertisement