Nyanya zaadimika Arusha

Wednesday March 13 2019

 

By Husna Issa, Mwananchi [email protected]

Arusha. Nyanya moja ya viungo muhimu vya chakula zimeadimika katika jiji la Arusha na hivyo kusababisha kupanda bei yake.

Kuadimika kwa nyanya katika masoko, kumetokana na maeneo mengi zinapolimwa nyanya kukumbwa na magonjwa wa mnyauko na kantangaze, hali ambayo imeshusha uzalishaji.

Wakizungumza na Mwananchi jana Jumanne Machi 12, 2019 baadhi ya wafanyabiashara wa nyanya pia walieleza kukosekana nyanya kunatokana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yamechelewesha kilimo cha nyanya.

Mfanyabiashara Resipigi Masawe, amesema wanatarajia huenda kuanzia mwezi wa saba, nyanya mkoani Arusha zikaanza kupatikana kama kawaida.

Masawe alisema hivi sasa nyanya zimepanda bei kutokana kwenda kununuliwa mikoa ya Singida, Dodoma, Iringa na mikoa mingine hivyo gharama zinapanda

kutokana na umbali.

Advertisement

Alisema sanduku la nyanya lilikuwa linauzwa Sh20,000 limepanda bei na kufikia Sh30,000 na la Sh35,000 limefikia Sh50,000 na kwamba nyanya moja kwa sasa wanauza kwa Sh500.

Mfanyabiashara mwingine Ndewario Mbise alisema kupanda kwa gharama za kilimo  kumesababisha kupanda pia bei za nyanya.

Mfanyabiashara Asha Salumu alisema bei zimepanda sana na sasa hawana faida tena ya biashara ya nyanya.

Asha aliendelea kusema kuwa changamoto nyingine ni pamoja na ubovu wa nyanya ambazo zinaponyeshewa na mvua huharibika.

Advertisement