VIDEO: Nywele bandia, leseni zazua mjadala Kilimanjaro

Muktasari:

  • Wananchi mkoani Kilimanjaro wamesema nywele bandia kuwekewa ushuru kutasababisha wengi kushindwa kumudu gharama huku wafanyabiashara wakilalamikia kukosa wateja.

Moshi. Wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2019/20 bungeni leo Alhamisi, maeneo mbalimbali katika mkoa wa Kilimanjaro watu walikuwa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.

Hali hiyo ni tofauti na miaka mingine ambapo ilizoeleka kuona watu katika mitaa mbalimbali wakiifuatilia katika makundi.

Pamoja na uwepo wa hali hiyo, baadhi ya wananchi wametoa maoni yao kuhusiana na serikali kupendekeza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye nywele za bandia.

Elizabeth Mushi amesema ushuru huo utasababisha bidhaa hizo kupanda bei na wengi wao kushindwa kumudu gharama hizo kutokana na ugumu wa maisha.

"Kwa hali ya maisha ilivyo  sasa tunapata ugumu kununua nywele hizo, sasa kama Serikali itaweka ushuru tena, tutashindwa kununua bidhaa hizo kabisa kwa sababu wauzaji nao watapandisha bei na kitakachofuata ni kwamba wengine tutalazimika kunyoa,"amesema Elizabeth.

Mmoja wa wafanyabiashara wa nywele bandia mjini Moshi, Nestory Assenga amesema Serikali kuweka ushuru kwenye nywele bandia kutasababisha wao kupandisha bei kwa wateja wao jambo ambalo litaongeza ukali wa maisha.

"Kwa hali ilivyo sasa, wateja wengi wanashindwa kununua nywele hizo kutokana na ugumu wa maisha, sasa kama Serikali  itaweka ushuru wateja wetu watapungua na biashara zitaendelea kuwa mbaya zaidi kutokana na ugumu wa maisha ulivyo kwa sasa, tunaomba Serikali iangalie namna nyingine ya kuwasaidia  Watanzania, "amesema Assenga.

Kuhusu leseni, baadhi ya madereva mkoani Kilimanjaro wameeleza kuwa suala la ongezeko la tozo za ada ya leseni za udereva kutoka 40,000 miaka mitatu hadi 70,000 kwa miaka mitano ni nafuu lakini tatizo litakuwa ni namna ya kuipata fedha hiyo kwa wakati mmoja kulingana na hali ya maisha ilivyo kwa sasa.

"Kiukweli 70,000 ni nafuu lakini kuja kuipata hiyo fedha ni mtihani mkubwa kutokana na maisha yalivyo magumu kwa sasa,"amesema Philipo Masunga.