TANZANIA ILIVYOSIMIKA MARAIS WA UGANDA- 8: Obote arejea madarakani, apinduliwa tena

Monday February 11 2019

 

Tume ya kijeshi iliyomwondoa Godfrey Binaisa madarakani ilisimamia uongozi wa Uganda kwa siku 10; kuanzia Mei 12 hadi 22, 1980, mwenyekiti wake akiwa ni Paulo Muwanga na makamu wake ni Yoweri Museveni.

Baada ya kuondolewa kwenye kiti chake cha urais, Binaisa aliendelea kukaa katika Ikulu ya Entebbe akisubiri kupelekwa watakakompeleka waliompindua. Hakukimbia kama wengine walivyofanya walipopinduliwa.

Baada ya siku chache kupita wakati akiwa Ikulu bila kujua la kufanya, aliondolewa na kupelekwa kwenye nyumba mo-ja mjini Entebbe.

Mwandishi A. Kasozi katika ukurasa wa 136 wa kitabu chake, ‘Social Origins of Violence in Uganda, 1964-1985’ ameandika: “Baada ya kupinduliwa, (Binaisa) alikuja ku-gundua kuwa katibu wake na mkuu wake wa usalama walikuwa ni wapelelezi wa Obote.”

Kupitia matangazo ya Redio Uganda, Muwanga alitangaza kuwa vyama vyote vya siasa nchini Uganda “sasa viko huru kuanza shughuli zake za kisiasa.”

Jumatatu ya Mei 12, 1980 Redio Uganda ilitangaza kuwa “Tume ya Kijeshi imetwaa madaraka ya urais ... Hiki ni kitendo cha Tume ya Kijeshi na si cha jeshi.”

Baadaye siku hiyo, kwa mujibu wa kitabu ‘Social Origins of Violence in Uganda, 1964-1985’ cha A. Kasozi, Muwanga akatangaza kuwa “kuchukua madaraka haya hakutahojiwa na mahakama yoyote.” Wajumbe wengine wa tume hiyo walikuwa ni Oyite Ojok, Tito Okello, Zed Maruru na Kanali William Omaria.

Kuanzia Mei 22 Tume ya Kijeshi ilikabidhi madaraka yake kwa Tume ya Rais ambayo ilisimamia kazi hiyo kuanzia hapo hadi Desemba 15, 1980 ulipofanyika Uchaguzi Mkuu nchini humo na matokeo kutangazwa.

Tume hiyo ilikuwa na wajumbe watatu tu ambao ni Saulo Musoke, Polycarp Nyamuchoncho na Joel Huunter Wa-cha-Olwol. Hata baada ya Tume ya Kijeshi kukabidhi madaraka yake kwa Tume ya Rais, Muwanga alikuwa na wadhifa wa uwaziri mkuu kwa siku 24; kuanzia Agosti Mosi hadi 25, 1980.

Uchaguzi Mkuu uliitishwa na kufanyika Jumatano ya Desemba 10, 1980 na chama cha Uganda People’s Congress (UPC) cha Milton Obote kilitangazwa kushinda na kiongozi huyo kurejea madarakani kwa mara ya pili. Waangalizi wa kimataifa walisema uchaguzi huo haukuwa huru wala wa haki.

Wapinzani wa UPC waliamini kuwa uchaguzi huo ulivurugwa ili kumsaidia Obote kushinda, hatua iliyomfan-ya Yoweri Museveni kuingia msituni na kuapa “kuishughulikia” Serikali ya Obote.

Juni 1981, Tanzania ilionyesha nia ya kuondoa askari wake wote waliokuwa wamebakia Uganda. Lakini Serikali ya Uganda haikuamini kama hilo lingetokea.

Wanajeshi wa Tanzania walipoanza kufanya maandalizi ya kuondoka Uganda, Serikali ya Uganda ikashtuka. Muwanga, ambaye sasa alikuwa Makamu wa Rais wa Uganda, na Okello, walikimbilia Dar es Salaam haraka kumpigia magoti Mwalimu Nyerere. Kwao huu ulikuwa ni wakati muhimu sana kwa usalama wa Uganda, lakini kwa Nyerere ilikuwa ni mzigo mkubwa wa gharama kwa Tanzania kuendelea kuyaweka majeshi yake Uganda.

Walipowasili Tanzania, Muwanga na Okello hawakufaniki-wa mara moja kuonana na Mwalimu Nyerere. Baada ya kusubiri sana, baadaye walimpigia simu. Walipompata kwa simu, Muwanga alijaribu kumshawishi akiomba waendelee kubaki kwa muda zaidi.

Nyerere alijibu, “Wanajeshi wa Tanzania wanarudi nyumbani.” Muwanga alizidi kumsihi Nyerere. Lakini Nyerere akasema hapana. Akamwomba angalau maofisa wa jeshi wabaki. Nyerere akasema hapana. Lakini akamwahidi kuwa atawabakiza wanajeshi 800 kuendelea kulifundisha jeshi la Uganda na kwamba watakuwa kwenye kambi ya mafunzo na si mahali pengine popote wala kujihusisha na jambo jingine lolote.

Kufikia mwishoni mwa 1981, suala la usalama likawa changamoto kubwa kwa Serikali ya Obote. Vurugu na mauaji yaliendelea.

Aliposhindwa kwenye uchaguzi mkuu, Museveni, akiwa na wenzake 27, waliunda jeshi la upinzani la kitaifa (NRA) na kuanzisha vita ya msituni. Februari 1981 alifanya shambulio la kwanza dhidi ya Serikali ya Obote.

Mchana wa Ijumaa ya Julai 26, 1985, Obote alianza kuhisi kuwa hali haikuwa shwari kwake na kwamba lolote lingeweza kumtokea. Gazeti ‘Los Angeles Times’ la Julai 28, 1985 limeandika, “…juzi (Ijumaa) Obote alitoa kiasi kikubwa cha fedha kutoka benki, inaonekana alitarajia kuwa saa za kukaa ofisini zilikuwa zinahesabika.”

Kwa mujibu wa kitabu cha ‘Obote: A Political Biography’ cha Kenneth Ingham, siku iliyofuata saa moja asubuhi akiwa ofisini kwake, alipewa habari na mtu wake wa karibu kwamba wanajeshi mjini Gulu walikuwa katika makundi makubwa wakiandamana kuelekea Kampala wakiongozwa na Basilio Okello.

Obote mara moja akajaribu kuwasiliana na maofisa waandamizi wa jeshi ambao walipaswa kuwapo kwenye viunga vya jiji la Kampala lakini hakuna hata mmoja ali-yepatikana isipokuwa Brigedia Smith Opon Acak, ambaye ni mwaka jana tu (Agosti 1984), alikuwa amemteua kuwa mkuu wa majeshi. Lakini hata alipopatikana hakuweza ku-toa msaada wowote kumwokoa bosi wake.

Obote akajaribu kuzungumza na kamanda wa vikosi vya jeshi vilivyokuwa Kampala, lakini akajibiwa kuwa kamanda huyo hakuwa ofisini. Kaimu wake, ambaye ndiye alipokea simu hiyo, alimwambia Obote kuwa aliteuliwa na Muwanga na kwa hivyo aliwajibika kwake tu na si kwa mtu mwingine awaye yote.

Kaimu kamanda wa kikosi hicho alimjibu Obote kwamba watu wote walioko chini yake wameshakimbia.

“Mipango yote ya kumpindua Obote iliandaliwa na Basilio Okello akishirikiana na maofisa saba au wanane,” kinaandika kitabu ‘The Raging Storm: A Reporter’s Inside Account of the Northern Uganda War 1986—2005’ cha Caroline Lamwaka.

Mshauri mkuu katika mpango huo ni mwanadamu aliyeit-wa Andrew Adimola. Mipango yote ilifanyika Gulu kwa wiki moja na utekelezaji wake ukaanza Jumatano ya Julai 24, 1985.

Jumamosi ya Julai 27, 1985, wakati Museveni akiwa Swe-den akisaka silaha, Obote alipinduliwa na makamanda wa jeshi lake Brigedia Bazilio Olara-Okelo na Jenerali Tito Okello. Katika matangazo ya Redio Uganda ya saa 5:30 asubuhi, sauti ilisikika ikisema “jeshi limekomesha kabisa utawala wa Obote wa kikabila.”

Tangazo hilo lilisababisha uporaji na milio ya risasi mitaani. Taarifa nyingine zikadai kuwa mara baada ya kupinduliwa, Obote alikimbia nchi. Makamu wake, Muwanga na mawaziri wake kadhaa nao walikimbia.

Jumatatu ya Julai 29, 1985, aliyekuwa mkuu wa majeshi ya Uganda, Luteni Jenerali Tito Okello, akaapishwa kuwa Rais mpya wa Uganda.

Wawili hawa Brigedia Olara-Okelo na Jenerali Okello waliitawala Uganda kupitia Baraza la Kijeshi (MC), lakini miezi michache baadaye, Jumapili ya Januari 26, 1986, Mu-seveni na jeshi lake la NRA akatwaa madaraka. Siku tatu baadaye, Januari 29, akaapishwa kuwa rais wa nane wa Uganda.

Advertisement