Ofisa Takukuru mbaroni akidaiwa kumbaka mtoto wa dada yake

Muktasari:

  • Ofisa wa Takukuru anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumbaka na kumlawiti mpwa wake.Hatua hiyo imekuja baada ya mpwa wake kuchoshwa na vitendo hivyo vya udhalilishaji na kutoa taarifa Polisi

Sumbawanga. Ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Rukwa, Jonas Jackson (34) anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumbaka na kisha kumlawiti mtoto wa dada yake aliyekuwa akiishi naye.

Ofisa huyo alikamatwa Februari 7, 2019 baada ya mtoto huyo kwenda kuripoti kituo kikuu cha polisi mjini Sumbawanga kufuatia kuchoka kufanyiwa vitendo hivyo.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa leo Jumatatu Februari 11, 2019 baada ya mlalamikaji mwenye umri miaka 18, kwenda polisi kutoa taarifa ya vitendo vya unyanyasaji anavyofanyiwa.

Msichana huyo amedai amekuwa akifanyiwa vitendo hivyo na mjomba wake tangu Septemba, 2018.

Amebainisha kuwa mtuhumiwa huyo mara kwa mara anapotoka kwenye starehe zake na kurejea nyumbani akiwa amekunywa pombe alikuwa na tabia ya kumnywesha pombe, kuanza kumbaka na kumwingilia kinyume na maumbile.

Kamanda Kyando amesema mtuhumiwa huyo anashikiliwa na polisi na muda wowote atafikishwa mahakamani.