Ofisa mifugo awekwa chini ya ulinzi Tabora

Kaimu Kamanda Takukuru Mkoa Tabora,Mashauri Elisante.picha na Robert Kakwesi

Muktasari:

 

  • Jeshi la Polisi mkoani Tabora linamshikilia ofisa mifugo katika manispaa ya Tabora, Cornellius Massawe kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kiwatoza wafugaji pesa ambazo haziingii serikalini

Tabora. Jeshi la Polisi mkoani Tabora linamshikilia ofisa mifugo katika manispaa ya Tabora, Cornellius Massawe kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kiwatoza wafugaji pesa ambazo haziingii serikalini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel  Nley amesema wanamshikilia Massawe kuanzia leo Jumatano Januari 23 kutokana na malalamiko ya wafugaji waliyoyatoa mbele ya Mkuu wa Mkoa na Naibu Waziri wa Mifugo, Abdallah Ulega kuwa wananyanyaswa na kutozwa fedha ambazo zinazokatiwa risiti zitakuwa pungufu.

"Tunafanya uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama kwa lengo la kutenda haki,"amesema.

Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tabora, Mashauri Elisante amesema suala la ofisa mifugo huyo bado halijafika kwao na kuwa wakilipata watalishughulikia.

Amesema Takukuru kuna wataalamu wa uchunguzi ambao watalishugulikia pasipo tatizo lolote na kubaini ukweli.

Afisa mifugo huyo amekamatwa leo kufuatia agizo la mkuu wa mkoa huo, Aggrey Mwanri baada ya malalamiko ya wafugaji kuwa anawanyanyasa na kuwatoza faini huku kiwango kinachokatiwa risiti kikiwa kidogo ukilinganiaha na pesa wanayolipa.